KAMPUNI ya TanzMED imezindua rasmi applikesheni mpya ya afya inayolenga kumuezesha Mtanzania kupata taarifa na huduma bora za afya moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa TanzMED , Mkata Nyoni, amesema App hiyo inapatikana kwenye App Store na Google Play, ambapo unaweza kuipakua na kujisajili bila gharama yoyote na kufurahia huduma mbalimbali zinazotolewa ikiwa inawezeshwa na akili mnemba (AI).
Amesema kupitia TanzMED, mtu anaweza kuzungumza na Madaktari Bingwa kwa njia ya video au kuchat. Pia, ataweza kupata huduma za afya ya akili kwa ushirikiano na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe, pamoja na nyenzo za afya ya wanawake, ikijumuisha afya ya uzazi na hedhi.
Aidha, Mtanzania anaweza kupata elimu kuhusu Ukimwi/VVU na huduma nyingine za afya, na kuweka miadi ya kukutana na daktari pamoja na kufika hospitali iliyo karibu na wewe.
“Lengo kubwa la kuanzisha TanzMED ni kuwawezesha Watanzania kuwa na afya bora kwa kukuleta huduma mbalimbali za afya kiganjani mwako. Pia, TanzMED inakuwezesha kuweka miadi na hospitali pamoja na kufika hospitali iliyo karibu na sehemu uliopo,” alisema Nyoni.
Tunatumia fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote kutembelea Google Play na App Store na kupakua app ya TanzMED bure kabisa na kufurahia huduma za afya kidigitali!.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED