RIPOTI MAALUM: Mifuniko ya 'mamantilie' inavyokaribisha saratani

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:49 AM Jul 24 2024
news
PICHA: JOHN BADI
Mamalishe akiandaa ugali kwa ajili ya wateja wake katika eneo la Mwenge, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam hivi karibuni.

MIFUKO ya plastiki imeshathibitika kisayansi ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu na viumbe wengine.

Serikali ya Tanzania ilishapiga marufuku kuzalisha, kusambaza, kuuza na kutumia mifuko hiyo tangu Juni Mosi, 2019. 

Hata hivyo, baadhi ya wapishi na hasa mamalishe na babalishe, wakiwamo wa mkoani Dar es Salaam, wanaitumia kuhifadhi chakula na hivyo kuziweka hatarini afya za walaji.

Mwandishi wa Nipashe amebaini baadhi ya wafanyabiashara hao wa chakula hutumia mifuko hiyo ama kupikia chakula au kuhifadhi chakula kama nyenzo maalum ya kuwezesha kiendelee kuwa na joto.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa mifuko hiyo inapopata joto katika chakula, inazalisha chembechembe ambazo ndio wakala wa kusababisha saratani.

Ni ufafanuzi unaotolewa na wabobevu wa eneo hilo la tiba, wakioanisha uzoefu, ushuhuda na yaliyomo katika utafiti mbalimbali.

Sharifa Mohamed, mamalishe katika Soko la Buguruni, jijini Dar es Salaam, anasema hutumia mifuko ya plastiki kufunika chakula chake anapomaliza kupika, akiamini inasaidia kutunza joto.

"Nikifunika kama hivi nikija kupakua, chakula kinakuwa cha moto. Mfuko huu (anaushika) hauyeyuki wala hautoi chochote, ni kama unavyoona, haujalainika, chakula kina moto," anasema Sharifa.

Mamalishe huyo anasema hajui kama mifuko hiyo si salama kiafya, akisisitiza yeye pia hula chakula hichohicho anachoandaa kwa ajili ya wateja, hata kikibaki baada ya kufunga biashara, hupeleka nyumbani kuliwa na wanafamilia.

"Hii mifuko si kwamba inayeyuka katika chakula, inabaki hivihivi. Mifuko hii ninaipata kwa wauzaji sukari, ule mfuko wa ndani ya mfuko wa sukari ndio ninachukua kwa ajili ya kufunikia chakula," anasema Sharifa.

Mamalishe huyo anasema huifua mfuko wa aina hiyo huutumia kwa kipindi cha hadi miezi mitatu, akiifua baada ya kazi.

"Baada ya miezi mitatu unaanza kuona mfuko huu umechoka, unatafuta mwingine, unabadilisha.

"Nikimaliza kuuza chakula, changu ninakwenda kuufua huu mfuko, ninauanika, kesho ninaendelea kufunikia tena chakula. Inanisaidia sana kuhifadhi chakula kiwe na joto," anasema Sharifa.

Mjasiriamali anayeuza mihogo ya kukaanga Buguruni, jijini Dar es Saalam, Brigita Kristian, anashauri serikali iwezesha upatikanaji vifungashio mbadala ambavyo vitawasaidia katika kufanya biashara.

"Mtu anakuambia niwekee mihogo mitatu, kachumbari na pilipili, ina maana ukimwekea katika vifungashio vya bahasha, inachanika na matokeo yake mihogo inadondoka.

"Hata hii mifuko laini ambayo tunawawekea wateja, inaungua. Inanibidi niweke miwili ninapohudumia mteja na bado tunapata shida," analalama mjasiriamali huyo.

Brigita anasema hana uelewa kama mifuko hiyo inasababisha mtu kuugua maradhi ya saratani.

"Kitu mbadala cha kutumia labda wateja wajinunulie kontena, nina baadhi ya wateja wangu wa hapa karibu huwa ninawawekea katika sahani zangu.

"Sasa kwa hawa wapitanjia, hawana kontena, inatubidi tuwawekee katika mifuko ya plastiki.

"Bado tupo kwenye wakati mgumu, hata hii mifuko ambayo imezuiliwa wametupandishia bei, hivi sasa inauzwa Sh. 1,500 wamepandisha kwa sababu imepigwa marufuku na ile mifuko ya bluu ukiweka vitu vya moto, kunatokea shida iileile, inayeyuka," Brigita anasema.

Mjasiriamali huyo anasema elimu inapaswa kutolewa kwa wananchi, wanapokwenda kununua chakula, wawe na chombo cha kubebea ili kuepuka vifungashio vya plastiki vyenye madhara kiafya.

Godfrey Minja, mfanyabiashara katika soko la Buguruni, anasema serikali inapopiga marufuku matumizi ya mifuko plastiki, iwezeshe upatikanaji vifungashio mbadala ambavyo ni rahisi kwao kuvipata na kuvitumia kulinda afya za walaji.

"Wamepiga marufuku mifuko ya plastiki lakini watu wanaendelea kuitumia. Je, mbadala wa hivi vifungashio ni upi ili tuache kuvitumia? 

"Kuna kipindi tunaambia aina fulani ya mifuko ndio inatakiwa na serikali baada ya muda hawaitaki tena. Wanatuchanganya sisi wananchi, hatujui serikali inataka ipi.

"Hivyo viwanda vinavyozalisha huenda ni vyao wenyewe viongozi wetu huko serikalini, unaweza kukuta mwanasiasa ana kiwanda chake hatuwezi kujua. 

"Hii mifuko ambayo imepigwa marufuku na serikali ndio inayozalisha fedha nyingi, inachafua mazingira lakini inazalisha fedha," mfanyabiashara huyo anadai.

HATARI YA SARATANI

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, Harrison Chuwa, anasema kuna uwezekano wa kupata saratani kutokana na matumizi ya mifuko ya plastiki katika kupika na kuhifadhi chakula.

Bingwa huyo anaeleza kuwa kwa Afrika, plastiki zinazozalishwa au kuingizwa barani, zikipata joto zinatoa vipande vidogo vya plastiki vyenye sumu.

"Mfano, kwa viumbe baharini wataalamu wamebaini samaki wakila plastiki, wanakufa au kuharibu mfumo wao wa chakula kutokana na hizo chembechembe za plastiki.

"Chembechembe hizo ni hatari kutokana na kuwa na kemikali ambazo zinatokana na plastiki zinapopata joto, kuna kemikali nyingi zinazotumika kutengeneza plastiki na kuzifanya ziwe laini. 

"Plastiki ni kama PVS ambazo ukiziona zinakuwa ngumu, ili kuifanya iwe laini, wanatumia kemikali ambazo ni hatari zinapoingia katika mwili wa kiumbe hai," bingwa huyo anasema.

Dk. Chuwa anasema aina nyingine ya kimekali huifanya plastiki hata ikianguka isipukutike, na kwamba kwa wanyama kemikali hizo zimethibitika zinaweza kusababisha saratani.

"Kuna utafiti ambao ulifanywa India miaka miwili iliyopita, waliona kuna ongezeko la saratani ya koo na ugumba kwa sababu kule hata chai wanakunywa kwa kutumia kikombe cha plastiki. Watafiti walianglia kama matumizi hayo ya plastiki yanachangia ongezeko hilo la wagonjwa," anasema Dk. Chuwa.

Hata hivyo, bingwa huyo anasema kuwa mpaka sasa hakuna utafiti unaoonesha moja kwa moja kwamba plastiki zinasababisha shida hiyo, ingawa maabara za wanyama zimeonesha kemikali mbili zilizomo katika plastiki zinaweza kusababisha saratani.

Ofisa Afya wa Jiji la Dar es Salaam, Reginald Mlay, anasema huwa wanatoa elimu katika masoko na kuzungumza na mamalishe na babalishe kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki katika kupika na kuhifadhi vyakula.

"Kubadili tabia za watu kunahitaji kuwa na muda wa kutosha kwenye suala zima la ubora na usalama wa chakula kinapoandaliwa hadi kumfikia mlaji, tuhakikishe kinafika katika hali ya usalama," anasema Mlay.

Ofisa Afya huyo anathibitisha kuwapo matumizi ya mifuko ya plastiki kuhifadhi na kupika chakula katika eneo lake la kazi. Anasema wanafanyia kazi changamoto hiyo kwa kutoa elimu.

Anasema kuwa mwaka 2021, kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), walitoa elimu kwa mamalishe katika maeneo yenye watu wengi jijini, akiyataja kuwa ni pamoja na Soko la Kimataifa la Samaki Feri, Ilala, Mnazi Mmoja, Karume, Buguruni, Tabata na Gongolamboto.

"Mifuko ya plastiki imethibitika kisayansi inatoa chembechembe ambazo zinapopata moto zinaweza kusababisha ugonjwa wa saratani baadaye.

"Watu wengi wanavyotumia hawaoni shida kwa sasa, kumbe ni tatizo linalojikusanya kidogokidogo, itafika wakati unaona fulani ana tatizo la saratani ya utumbo, utumbo mkubwa, kwenye midomo, mikono, mguu kutokana na tatizo hilo," anaonya Mlay.

Ofisa huyo anasema mamalishe na babalishe wanaweza kutumia vifungashio mbadala wa bahasha na foili katika kuhifadhi vyakula vya moto ili kulinda afya ya mlaji.

Anasema maeneo mengi wanatumia foili kufunga vyakula na upatikanaji wake kwa sasa ni gharama nafuu, hivyo wanaweza kutumia ili kulinda afya za wananchi.

Katazo la mifuko ya plastiki ni utekelezaji wa kifungu cha 230(2)(f) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.  

Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, tani 350,000 za mifuko ya plastiki huzalishwa kila mwaka. 

Hata hivyo, baraza hilo linabainisha kuwa chini ya asilimia 10 ya mifuko iliyotumika hurejereshwa, likiwa na angalizo pia kwamba mifuko ya plastiki huchukua miaka 400 mpaka 1,000 kuoza ardhini.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Mwaka 2018 kuhusu madhara ya mifuko hiyo, inaonesha viumbe wa majini wanaathiriwa na hata kufa kutokana na kuingia kwa bidhaa za plastiki baharini. 

Meneja wa NEMC Kanda ya Temeke, Anord Mapinduzi, anaungana na wataalamu waliotangulia kwamba, wananchi wanaweza kupata magonjwa ya saratani kutokana na matumizi ya mifuko hiyo katika kupika au kuhifadhi chakula.

Anasema mifuko hiyo ina kemikali aina ya Bispheno 4 ambayo anaitaja ni hatari kwa afya za binadamu, hususani kwa wanaotumia mifuko hiyo katika kupika au kuhifadhi chakula ili kiendelee kuwa na moto.