RIPOTI MAALUM Madhila unyanyapaa kwa wenye ualbino kujifungua

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:20 AM Jul 26 2024
Clara Majaliwa (34), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam.
Picha: Maktaba
Clara Majaliwa (34), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam.

BAADHI ya Watanzania wenye ualbino wamelalama kunyanyapaliwa wanapokwenda zahanati, vituo vya afya na hospitalini kupata huduma za uzazi.

Tazama mkasa huu unaosimuliwa na Clara Majaliwa (34), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam ambaye ni miongoni mwa wenye ualbino nchini:  

"Siku niliyokwenda katika jengo la kuhudumia wajawazito kuanzia kliniki katika hospitali ya... (anataja jina la hospitali), nilikuwa na shauku kubwa, lakini nilikumbana na unyanyapaa wa hali ya juu ambao sikuutarajia. 

"Nilipoingia tu katika lile jengo, kundi kubwa la kinamama wajawazito lilinigeukia, kila mmoja ananiangalia na kunishangaa huku wakinong’onezana na wengine kutikisa vichwa, wakionesha ishara zote za kunionea huruma.

 "Nilijisikia vibaya lakini nikajikaza, ikabidi nitembee huku nikiwa nimeinamisha kichwa changu mpaka alipokuwa mtoahuduma za afya ya uzazi ili kuelekezwa utaratibu." 

"Muuguzi aliponiona, naye akahamaki na kuniambia maneno yaliyogeuka maumivu makubwa moyoni mwangu.

 "Alitamka 'yaani na wewe umebeba mimba? Haujihurumii kwa hali yako ya ualbino? Hivi huwa mnafikiria nini nyie watu? Sasa wakati wa kujifungua itakuwaje?'" 

Mama huyo wa watoto watatu ambao hawana ualbino, anasema kauli ya muuguzi ilimfanya aogope na kujutia uamuzi wake wa kubeba ujauzito, hata akahisi yeye kubeba ujauzito ni kukaribisha kifo.  

Clara anasema mama yake mzazi alifanya kazi kubwa ya kumweka sawa kisaikolojia ili aendelee na safari yake ya kliniki. 

"Mama yangu aliniambia kuwa si kweli kwamba kwa kubeba ujauzito ningekufa kwa sababu alikuwa ameshuhudia wanawake wengi wenye ualbino wakijifungua salama, hivyo akanitaka nisiogope," Clara anasema. 

Clara anasema kuwa mwezi uliofuata aliamua kubadili hospitali, alikwenda hospitali nyingine ya serikali kuanza upya kliniki ili kuepuka maneno ya kuudhi yaliyotolewa dhidi yake alipokwenda hospitali ya awali, lakini huko kwenye hospitali ya pili nako mambo yakawa hivyo hivyo. 

"Baada ya kukumbana na madhila hayo, niliamua kujikaza, nikaendelea na kliniki katika hospitali hiyo ya pili hadi nilipojifungua.  

"Cha ajabu ni kuwa, baada ya kujifungua, manesi waliitana na kuzunguka kitanda changu, wakimshangaa mtoto wangu aliyetoka na rangi nyeusi ilhali mimi nina ualbino. 

"Ile siku niliyojifungua nilikuwa kama kivutio cha hospitalini. Kila baada ya dakika chache, nesi mpya anakuja kumwangalia mtoto na kuniuliza maswali ya karaha kama vile 'mume wako ni kama wewe (yaani mwenye ualibino)? Clara anasimulia. 

Clara anasema alipitia madhila ya aina hiyo katika miaka minane ya safari yake ya uzazi wa watoto watatu iliyoanza mwaka 2014 hadi 2022. 

Mama huyo anaeleza kuwa kama asingekuwa na mshauri wa mama yake mzazi, pia elimu ya darasani (msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Miradi), asingehudhuria kliniki na angejifungulia nyumbani.

 Si Clara tu aliyekumbana na unyanyapaa huo. Asha Boniface, mwenye ualbino, anasema hatosahau siku aliyokwenda kutoa kijiti cha uzazi ili kubeba ujauzito wa mtoto wake wa pili katika moja ya hospitali za serikali mkoani Dar es Salaam. 

Asha anadai kuwa nesi aligoma kumpa huduma kwa maelezo kuwa amsubiri nesi mkuu "kwa kuwa ngozi yake ni nyeti sana". 

Mama huyo wa watoto wawili anasimulia, "Siku hiyo nilikwenda kwa ajili ya masuala ya uzazi wa mpango, nesi niliyemkuta aliniambia 'suala lako ni tofauti na wengine kwa sababau ngozi yako ni ‘sensitive’ (nyeti), ngoja mkuu wa kitengo aje kunisaidia kwa sababu sitaki kesi. 

"Nilikwenda kusubiri kwenye benchi kwa saa tatu bila msaada wowote mpaka mume wangu alipokuja na kunishauri twende hospitali binafsi." 

Patrick Leonard, mkazi wa Dar es Salaam anayejitambulisha kuwa mkewe anayemtaja kwa jina moja la Dorice, ana ualbino, anasema maneno ya manesi anapomsindikiza kliniki mkewe huyo, yanafanya ajisikie vibaya.

 Leonard anasema kila wanapohudhuria kliniki, anahisi kuhukumiwa kana kwamba amemwingiza mkewe huyo katika shida.

 "Mfano, niliwasikia wakimwuliza mke wangu, 'mtoto amefanana na baba yake? Baba yake rangi gani?' Walikuwa wanauliza tu kinafiki ili kujua rangi ya baba yake. Kama ningekuwa simpendi mke wangu ningeshamkimbia," analalama Leonard.

 Mary Kijagwa, mkazi wa Dar es Saalam, pia analalamika kunyanyapaliwa kutokana na kuwa na ualbino alipokwenda hospitalini jijini kupata ushauri wa njia ipi sahihi ya uzazi wa mpango atumie.

 "Maneno ya ajabu yalitolewa dhidi yangu. Tulishazoesha akili zetu kuvumilia maneno ya unyanyapaa mitaani kwetu, sikutegemea yatolewe katika vituo vya afya ambako kuna wahudumu wasomi," anasema.

 Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) linasema si hao tu waliopitia changamoto hiyo ya kunyanyapaliwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. 

 Utafiti wake uliofanywa kwa kushirikiana na Shirika la Handicap International kuhusu Hali ya Haki za Watu Wenye Ulemavu nchini, ulibaini mambo linayoyaita "ya kushangaza".

 Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo, katika mikoa 13 ukiwamo wa Dar es Salaam, asilimia 55 ya watu wenye ulemavu walikiri hukumbana na changamoto wanaposaka huduma za afya, wanawake wakiongoza kwa kunyanyapaliwa.

 Hali hiyo inakinzana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010 ambayo katika kifungu cha 26(2) inaelekeza kutoa haki kwa kundi hilo kupata huduma za afya bila kubaguliwa au kunyanyaswa.

  Vitendo hivyo pia vinakiuka Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inaelekeza kuwa, "Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria."

 Vilevile, Katiba hiyo, Ibara ya 13(4) inaelekeza kuwa, "ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote ile inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi."  

Mweka Hazina wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Abdilah Omary, anathibitisha kuwa na taarifa kuhusu kundi hilo kunyanyapaliwa katika baadhi ya maeneo ya kutolea huduma, hasa kwenye hatua ya uzazi. 

Anasema wengi wao wanapokwenda hospitalini, wanachukuliwa katika dhana tofauti kwamba hawakustahili kubeba ujauzito au kutumia njia za uzazi wa mpango kutokana na hali yao ya ngozi. 

"Kauli nyingine zinakatisha tamaa kwa watu wenye ualbino, 'mwanamke atajifunguaje ngozi yake laini, atachanika mwili mzima'," Omary anasema akinukuu baadhi ya dhana dhidi ya kundi hilo. 

Alisema kuwa hali hiyo inawatia hofu baadhi yao, akionya kuwa ni kauli zinazovunja na kukiuka haki za msingi za binadamu. 

Omary anashauri serikali iendelee kutoa elimu dhidi ya mitazamo hasi kwa watu wenye ualbino na isisitize watu kuchangamana bila kubaguana kutokana na maumbile hasa vijijini ambako anadai ndiko watu wanahitaji zaidi elimu hiyo. 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maisha ya Amani kwa Watu Wenye Ulemavu, Sofia Mbeyela, anasema malalamiko mengi wanayopokea, yanatoka vituo vya kutolea huduma za afya, hasa huduma za uzazi. 

"Baadhi ya madaktari na watoahuduma wengine wa afya wana mtazamo hasi kuhusu watu wenye ualbino, lakini nilichogundua wengi wao hawana elimu, na wanafanya kazi hiyo pasi na kuwa na wito au wanapuuzia miongozo ya Wizara ya Afya, hivyo niwaombe tu wabadilike," Amani anasema. 

Daktari katika Hospitali ya Magomeni, Patric Boniface, ananyooshea vidole baadhi ya watumishi wenzake wa kada hiyo, akieleza kuwa wapo baadhi ya wauguzi wenye tabia ya kunyanyapaa wagonjwa, akionya kuwa ni vitendo hivyo kinyume cha maadili yao ya kazi.  

"Tunapokuwa tunasoma kumhudumia binadamu, tunafundishwa kwa kila aina ya mgonjwa. Mimi nipo tayari kuhudumia mtu wa kundi lolote, inapotokea muuguzi anamnyanyapaa mwenye ulemavu, hiyo inakuwa ni tabia yake binafsi," anasema Dk. Boniface. 

Mratibu Huduma za Afya ya Uzazi Mama na Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Agnes Mgaya, anasema wameweka mfumo wa kupokea malalamiko dhidi ya mienendo ya watoahuduma za afya, ukijumuisha mabango yenye namba za mganga mfawidhi wa kituo na namba ya simu ya huduma kwa wateja inayopokewa na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) moja kwa moja. 

Hata hivyo, Agnes anasema hajapokea malalamiko rasmi kuhusu mtu mwenye ualbino kunyanyapaliwa na watoahuduma. 

"Inapotokea mtu yeyote, bila kujali rangi yake ya ngozi, ananyanyapaliwa, ana haki ya kufikisha malalamiko sehemu husika ili kusaidiwa na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya aliyemnyanyapaa," anasema Agnes. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, anaungana na TAS kushauri serikali na wadau wa haki za binadamu waendelee kutoa elimu kwa watoahuduma na jamii kuhusu ulemavu. 

Dk. Anna pia anashauri kufanyike ufuatiliaji wa vitendo vya unyanyapaa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuwafikisha wahusika katika vyombo vya haki ili wengine waone mfano na kubadilika. 

"Sera ya Afya izingatie haki na mahitaji ya kundi hili (watu wenye ulemavu). Tatizo kubwa ni jamii kutokuwa na uelewa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, ikiwamo uzazi kwa wanawake wenye ulemavu. Pia kuna utekelezwaji hafifu wa sheria zinazohusu kundi hilo. 

"Kisheria mwanamke mwenye ulemavu ana haki kama mwanamke mwingine yeyoye. Tofauti ni kuwa wanawake wenye ulemavu wana changamoto nyingi zaidi," Dk. Anna anasema. 

Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, yaliyonesha kuwa Tanzania ina watu wenye ulemavu 2,641,802. Kati yao, wenye ualbino ni 16,477 sawa na asilimia 0.04; Dar es Salaam ikiongoza kwa kuwa na na wenye ualbino 1,637.