Mke adaiwa kumuua mumewe kwa kumng’ata ulimi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:25 PM Apr 02 2024
Julius Rubambi akiwa na mkewe, enzi za uhai wake.
PICHA: MAKTABA
Julius Rubambi akiwa na mkewe, enzi za uhai wake.

OFISA Kilimo wa Kata ya Neruma katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Julius Rubambi (38), ameuawa kwa kile kinachodaiwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali, pamoja na kung'atwa ulimi; huku Elizabeth Stephen (36) ambaye ni mke wa marehemu, akituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mara, ACP Salim Morcas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema kuwa tayari mwanamke huyo yupo chini ya ulinzi na uchunguzi unaendelea, huku mhusika akiendelea kupata matibabu katika hospitali ya Kibara ambako amelazwa baada ya kujeruhiwa vibaya.

Hata hivyo bosi huyo wa Polisi mkoani Mara, hakuweka wazi kiini cha majeraha hayo, wala kuelezea kwa undani mkasa mzima wa tukio hilo, hata hivyo ameahidi kufanya hivyo mara upelelezi utakapo kamilika.

Kwa mujibu wa Kamanda Morcas, inadaiwa kuwa chanzo cha ugomvi huo unaodaiwa kusababisha mauaji ya ofisa huyo kuwa wivu wa mapenzi ambapo inaelezwa kuwa marehemu alimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano mengine nje ya ndoa.