'Ni mwendo wa kujenga sekondari kila kijiji'

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:41 PM Apr 02 2024
Profesa Sospeter Muhongo (mwenye suti katikati), katika picha ya pamoja na walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa serikali alipokabidhi mifuko ya saruji kuendeleza ujenzi wa Bukwaya Sekondari.
MPIGAPICHA WETU
Profesa Sospeter Muhongo (mwenye suti katikati), katika picha ya pamoja na walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa serikali alipokabidhi mifuko ya saruji kuendeleza ujenzi wa Bukwaya Sekondari.

UNAWEZA kusema huu ni mwamko mpya wa elimu katika jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara, ambapo baadhi ya vijiji katika kata 21 za jimbo hilo, vimeamua kujenga sekondari, kwa lengo la kusogeza elimu karibu na kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembeza umbali mrefu.

Kijiji cha Nyegina, Kata ya Nyegina, ni miongoni mwa vijiji vinavyojenga sekondari ambayo imepewa jina la Bukwaya, ikiwa ni ya pili kwenye kata hiyo, ikitanguliwa na Mkirira Sekondari.

Kwa upande mwingine, Kijiji cha Wanyere ambacho kiko katika Kata ya Suguti, nacho kinajenga sekondari yake ambayo itakuwa ni ya pili kwenye kata hiyo ikiwa imetanguliwa na ile Suguti Sekondari.

Aidha, wakazi wa Kijiji cha Nyasaungu Kata ya Ifulifu, nao wanajenga sekondari katika kijiji chao, huku wakazi wa Kijiji cha Muhoji katika Kata ya Bugwema nao wakijenga sekondari ya kijiji hicho.

Kwa mujibu wa mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, kata hiyo ina sekondari iitwayo Bugwema, lakini pia, Kijiji cha Kurwaki katika Kata ya Mugango nacho kinajenga sekendari yake iitwayo Profesa Massamba Memorial.

Kata ya Nyamurandirira nayo kwa sasa ina sekondari mbili baada ya kujengwa nyingine ya Seka Sekondari iliopo Kijiji cha Seka ikiwa imetanguliwa na Kasoma Sekondari.

Lakini pia amesema, awali Kata ya Nyakatende ilikuwa na sekondari moja iitwayo Nyakatende, na kwamba Kijiji cha Kigera katika kata hiyo kilishakamilisha ya pili iitwayo Kigera Sekondari.

"Wiki iliyopita nilitembelea Bukwaya Sekondari ambayo ilianza kujengwa mwaka 2022 na kukuta kuna mapungufu mengi, lakini wanavijiji wa Kata ya Nyegina wameamua kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya shule hii," Prof. Muhongo amesema.

Amesema katika uamuzi huo, wamepanga kuwa ifikapo Aprili 30 mwaka huu, madarasa mawili yawe yameezekwa, na kwamba yeye amekabidhi saruji mifuko 150 iliyonunuliwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo.

"Binafsi nimepanga kwamba ifikapo Julai mwaka huu, nitaendesha harambee ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi, ambayo ni fizikia, kemia na bailojia katika sekondari hiyo," amesema.