Miili ya wanawake yakutwa imetupwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:57 AM Jul 24 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya.

MIILI ya wanawake wawili imekutwa katika Mtaa wa Chinyika, Kata ya Mkonze jijini Dodoma, huku mmoja ukidaiwa kuwa na majeraha, ukiwa umefungwa katika mfuko wa plastiki, boksi na kiroba.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili huo umeonekana ukiwa na majeraha yanayotoa ishara ya kudhuriwa kwa kitu chenye ncha kali.

Akizungumzia tukio hilo juzi, Mwenyekiti wa mtaa huo, Aloyce Maswikwi, alisema matukio hayo yalitokea katika mtaa wake kati ya juzi na jana. Mmoja kati ya wanawake hao hajatambulika.

"Inaonekana aliyemuua alikwenda kununua godoro, akatoa nailoni ya lile godoro, akamfunga na nguo, akamchomeka katika mfuko na kisha kumfunga na mpira. 

"Pia alitafuta maboksi, akamlaza marehemu akamfunga na mipira hii ya bodaboda, mzigo umefungwa kweli kweli. Mimi na macho yangu ninaona," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa baada ya hapo, muuaji alichukua kiroba cha kuhifadhi mahindi cha madebe saba, akamweka na kisha kufunga na mpira. 

Alisema mzee mmoja aliyetoka kuchunga mifugo yake, alikwenda katika korongo hilo kwa ajili ya kunywesha ng’ombe wake, aliona kitu kama mzigo wa mtumba ukiwa umetupwa katika eneo hilo.

"Akamwita mwenzake, 'njoo tuangalie, kuna mzigo gani?' Alipokwenda wakasema 'ngoja tufungue kuna nini', hali iliyowafanya kuchana, walipokuwa wamechana waliona miguu ya mtu," alisema.

Mwenyekiti huo alisema walichana mfuko kisha boksi, mfuko wa godoro na kukutana na nyayo za mtu, hali iliyowafanya kuruka kwa mshtuko kwa kukuta mtu badala ya mzigo wa mtumba kama walivyokuwa wamefikiria awali.

Maswikwi alisema watu hao walipiga kelele zilizowafanya watu kukusanyika na kuwaita polisi ambao walifika na kuondoa mwili wa mwanamke huyo katika mifuko, nailoni na maboksi uliyokuwa umefungwa.

“Wakatuambia tuangalie kama tunamfahamu, tulipiga foleni wanawake kwa wanaume, tukamwangalia yule dada (ana umri wa miaka kama 20 hivi), kwa kweli hatukumtambua, hivyo askari wakamchukua," alisema.

Akielezea tukio la pili, Maswikwi alisema majira ya saa 12.00 asubuhi juzi, alipigiwa simu na askari kata akimweleza kuwa kuna msiba katika nyumba ya familia ya Careen Ndondo na hivyo aliamua kwenda eneo la tukio.

“Nilipofika nikakuta kweli amelala  mlangoni, wamemfunika kwa shuka, watu wengi wanalia, nikauliza 'vipi?', nikaambiwa kuwa wamemkuta ametupwa hapo alikuwa hana nguo," alisema.

Alisema walimwita mama wa marehemu, ambaye alieleza kuwa mwanawe alikuwa anafanya naye biashara ya nyanya sokoni, alimtoroka muda kidogo na hakufahamu alikokwenda.

"Alinieleza alikokwenda (marehemu) hajui na wala ndugu zake hawafahamu ila kuna rafiki yake anaitwa Mwache ambaye waliolewa wote Zuzu, ndiye anayefahamu alipo kama kuolewa, kaolewa na nani na ndiye anayetumiwa kuleta matumizi ya mtoto nyumbani," alisema.

Maswikwi alisema walipomwangalia, hakuwa na jeraha lolote mwilini na hivyo hawajui ni nini kilichosababisha kifo chake. 

"Yule dada watakuwa wamemuua huko mbali, wakaona waje wamtupe hapa Chinyika inaonekana kama ni ukatili fulani, matukio haya ni mazito. Nitoe wito kwa polisi waongeze juhudi katika kazi yao na hawa watu wakibainika watoe adhabu zinazostahili," alisema. 

Mama wa marehemu, Careen Ndondo alisema mwanawe aliondoka wiki nne zilizopita bila kumuaga anakoelekea lakini ilipofika saa 11.00 asubuhi juzi mjukuu wake alimweleza kuwa mama yake mdogo (Alice), amelala kwake na anapomwita haitiki.

"Tukainuka na kaka yake tukaenda pale na kumkuta kalala chali, tukasema msimshike, mtafuteni mwenyekiti lakini alipokuja ndugu yake mwingine alimshika na kumtingisha. Hata hivyo, alimkuta kakauka, nikasema huyu amekufa, siyo mzima," alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopistha Mallya, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo mawili. Uchunguzi unaendelea.

“Kweli matukio hayo yametokea lakini la huyo mmoja ambaye alifungwa katika kiroba anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30, hajafahamika, hivyo nitoe wito kwa watu kuja kumtambua ili hatua nyingine zichukuliwe," alisema. 

Mapema mwezi huu, katika Kata ya Nzuguni, jijini hapa, wasichana wawili walikutwa wameuawa ndani ya chumba walichokuwa wanaishi baada ya kupigwa na baadaye miili yao kuchomwa moto na watu wasiojulikana.