Mchinjita: TAKUKURU itupie jicho fedha za TASAF Ruvuma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:40 PM Jul 26 2024

 Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, ametoa wito kwa Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma na Wilaya ya Songea, Faustine Mpakiri, kufuatilia mfumo wa utoaji wa pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani hapo.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati  akihutubia wananchi na viongozi wa Songea, mkoani Ruvuma. Alisema kumekuwa na matatizo, ambapo maofisa wanashindwa kuwapa fedha watu waliojiandikisha kwenye TASAF msaada wanaostahili.

Mchinjita alisisitiza kuwa sehemu kubwa ya pesa za TASAF zimekuwa zikiibiwa, na hivyo kuna umuhimu mkubwa wa TAKUKURU kuingilia kati ili kubaini tatizo lilipo, kama walivyofanya mkoani Lindi, ambapo waliojiandikisha walipata haki zao wanazostahiki.

Aidha, Mchinjita alitangaza kuwa ACT Wazalendo wameanzisha SACCOS kwa ajili ya kuwasaidia wanachama wao kukabiliana na mikopo yenye riba kubwa, ambayo ni changamoto kubwa kwa wananchi. Alieleza kuwa Shushatanga SACCOS inafanya kazi kwa njia ya mtandao na ina usalama wa kutosha katika urejeshaji wa mikopo. Sharti kuu kwa wanachama ni kuwa na wadhamini wawili ambao pia ni wanachama wa ACT Wazalendo.