Ma-RC, ma-DC wawekwa kitanzini utekelezaji miradi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:06 AM Jul 24 2024
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie miradi yote ya maendeleo katika mikoa na wilaya zao na kuhakikisha inakamilishwa ili itoe huduma kwa wananchi.

"Kwenye eneo la usimamizi wa miradi, wakuu wa mikoa hakikisheni mnazo taarifa za utekelezaji miradi hiyo; hii ni fursa yenu ya kujua benki tuliyonayo ya utekelezaji miradi yote ya tangu mwaka 2021. 

"Angalieni ni miradi gani imepata fedha, na mjiridhishe kama imekamilika au la, na kama haijakamilika, fuatilieni ni kwanini haijakamilika," ameagiza.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo juzi wakati akizungumza na Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mikoa kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mtandao akiwa ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni jijini Dar es Salaam.

Majaliwa alisema miradi inayojengwa kwa fedha za serikali katika halmashauri na manispaa ni mingi, hivyo akasisitiza ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba mwaka huu ili ianze kutumika.

"Matumizi ya miradi hii ndiyo faraja kwa wananchi na ndiyo matamanio yao," alisema Waziri Mkuu, akitumia fursa hiyo kuhimiza viongozi hao wafuatilie uzalishaji chakula ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na ziada ya kutosha. 

"Tanzania tumezalisha chakula kingi na tuna ziada; wakuu wa mikoa na wilaya jukumu lenu kusimamia kilimo na uzalishaji uwe umefikia malengo na wenye ziada. 

"Pia fanyeni sensa ya kujua mazao katika maghala, uhifadhi wake ni mzuri, na je, kinatosha? Tuwe na takwimu za kutosha kuhusu chakula tulichonacho katika hifadhi yetu," aliagiza. 

Waziri Mkuu pia alisisitiza makusanyo yote ya fedha katika halmashauri na manispaa ni lazima yaingizwe benki ndipo yapangiwe matumizi. 

"Hata kama ni fedha za msaada kutoka taasisi au asasi zisiso za kiserikali, ni lazima DC ajue ili atoe taarifa kwa RC. Ma-RC wasimamie mtiririko wa fedha katika halmashauri.

"Suala la usimamizi wa mapato ya serikali liwe ajenda ya kudumu. Tusipofanya hivyo, tutashindwa kutekeleza mipango yetu.

"Mmemsikia Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuhusu ukusanyaji mapato, mapato ambayo baadaye yanaletwa katika maeneo yenu ili kutekeleza miradi," aliagiza.

Maeneo mengine aliyoyawekea msisitizo wakati wa kikao hicho ni pamoja na utatuzi wa kero za wananchi, udhibiti na uhifadhi wa mazingira, nishati safi ya kupikia, ulinzi na usalama, kilimo cha umwagiliaji, magonjwa yasiyoambukiza, maandalizi ya AFCON 2027 na ushirikiano baina ya viongozi wa serikali na wa CCM.

Kikaokazi hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.