Korti yasimuliwa mama, mwana walivyoua binti

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 09:02 AM Jul 24 2024
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Picha: Mtandao
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa mama alivyomuua mtoto wake, Beatrice Magombola, kwa kumchoma kisu katika titi la kulia kwa kushirikiana na mtoto wake wa kiume, Alphonce Magombola ili asitoe ushahidi mahakamani katika kesi ya nyumba ya familia.

Inadaiwa kuwa Machi 16, 2020, saa nne asubuhi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhani Kingai, alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu utata wa kupotea kwa Beatrice.

Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali Asiath Mzamiru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo wakati akiwasomea washtakiwa hao maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Akisoma maelezo hayo, Mzamiru alidai msiri huyo alidai kumekuwa na taarifa za utata kuhusu kupotea kwa binti huyo kwa kuwa mama mzazi wa Beatrice aitwaye Sophia Mwenda, anadai mtoto wake alikwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine alidai binti yake alikwenda Canada kutibiwa.

Hata hivyo, alidai mama huyo hakuweka wazi ugonjwa unaomsumbua Beatrice na taarifa za ugonjwa hazikuwa zikifahamika kwa ndugu wa Beatrice wala baba yake mzazi isipokuwa kaka yake mkubwa, Alphonce.

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa msiri huyo alidai Beatrice alikuwa na gari aina ya Vangard lililokuwa linatumiwa na Alphonce na pia nyumba yake iliuzwa na Sophia na kuna wakati washtakiwa hao wakihojiwa kupotea kwa Beatrice wanakuwa wakali.

"Kutokana na taarifa hizi za msiri, Kamanda Kingai alielekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi na upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kukamatwa kwa washtakiwa hawa," alidai Wakili Mzamiru wakati akiendelea kusoma maelezo hayo.

Pia inadaiwa kuwa wakati washtakiwa wanachukuliwa maelezo ya onyo, walikiri kumuua Beatrice kwa kumchoma kisu katika titi la kushoto, Alphonce alimfunga miguu na kumshika mikono ndipo Sophia alimchomachoma kwa kisu hadi alipofariki dunia.

"Baada ya kumuua, washtakiwa waliuzungushia shuka mwili na mkeka wa kichina na kwenda kuutupa eneo la Zinga, Bagamoyo," alidai wakili huyo.

Ilidaiwa mahakamani huko kuwa sababu ya kumuua ni kutokana na Beatrice kutaka kwenda kutoa ushahidi mahakamani Mbeya katika kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao.

Baada ya upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa maelezo hayo, ulidai utakuwa na mashahidi 40 na vielelezo 13.

Katika kesi hiyo, inadaiwa washtakiwa kwa pamoja walimuua Beatrice Desemba Mosi, 2020 huko Kijichi, Temeke, mkoani Dar es Salaam.