RIPOTI ya Hali ya Vyombo vya Habari ya 2022/2023, imekuja na mapendekezo matano yanayogusa maeneo ya marekebisho ya sheria, kuongeza uraghibishi, kuwa na mijadala ya kitaaluma, vyombo vya habari kuwa na sera ya jinsia na mabadiliko ya sera ya habari na utangazaji itungwe kwa pande zote za Muungano.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi uliopita na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ilihusisha upande wa Tanzania Bara na Visiwani, ikihusisha mahojiano na wadau wa sekta ya habari na nyaraka mbalimbali zinazohusika na uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa taarifa na uhuru wa vyombo vya habari.
Katika utafiti huo wanapendekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, zinapaswa kufanya mabadiliko ya sheria zinazosimamia sekta ya habari kwa ajili ya kutengeneza mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kutekeleza taaluma yao ipasavyo.
Aidha, wadau wa habari na wanaharakati wengine waimarishe uraghibishi kwa kusukuma mabadiliko ya sheria za habari, ikiwamo kutungwa kwa sheria rafiki kwa mazingira ya utendaji wa vyombo hivyo.
Pia, taasisi za kitaaluma za waandishi wa habari zikiongozwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), waanzishe mjadala na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo vya uandishi wa habari kwa ajili ya kupata suluhisho la kwanini kunakuwa na wanataaluma ‘wasioiva’ vyema ambao wengi wameshindwa kuhamisha walichofundishwa kwenye vitendo.
Matokeo ya utafiti kwa Tanzania Bara, yanaonyesha kuwa tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 2021, amekuwa na maneno na matendo yaliyoifanya tasnia ya habari kuaminiana na kufanyakazi katika mazingira rafiki yasiyoumiza waandishi wa habari.
“Ingawa maneno na matendo ya Rais Samia ni rafiki kwa waandishi wa habari, lakini bado sera, sheria na kanuni ni zile zile, bado kuna matukio ya waandishi wa habari kukamatwa na kunyanyaswa na mamlaka, kunyimwa taarifa. Tunaona kwa mazingira haya kama sheria zitaendelea kuwa zile zile na kukwaza uandishi wa habari,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Aidha, ripoti hiyo inabainisha kuwa pamoja na hatua chanya zilizopigwa ikiwamo kufunguliwa magazeti yaliyokuwa yamefungiwa, kukutana na wahariri, na licha ya kauli za matumaini za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (wakati huo), Nape Nnauye.
Kwa sasa Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 iko katika mapitio huku kukiwa na matumaini chanya kwa wadau kwa kuwa itasaidia kuwa na sheria nzuri.
Kuhusu uwekezaji na umiliki, hakuna uwekezaji mpya kwa kuwa bado umiliki uko mikononi mwa wachache na kuwa na nguvu ya ushawishi huku wakifurahia mazingira wezeshi yaliyowekwa na Rais Samia, kukiwa na tatizo kubwa la uendelevu kwa vyombo vyote vya mtandaoni, magazeti, radio na TV.
“Utafiti unaonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa tekonolojia, kubadilika kwa sheria na kanuni, ushindani kwa walaji uliosababishwa na kuwapo kwa mitandao ya kijamii, kubadilika kwa mazingira ya biashara na walaji, uwekezaji mdogo na matangazo kutumika kama mbinu ya kuumiza uandishi wa habari. Tunaona ni muhimu vyombo vya habari vikawa na ubunifu kwa kuwa na vyanzo tofauti vya mapato,” inabainisha ripoti hiyo.
Aidha, vyombo vya habari vimekuwa vikipata msaada kutoka kwa wadau mbalimbali huku wengi wakiwa na vipaumbele vyao na mahali wanakoelekeza fedha wanazotoa.
Jingine ni mafunzo kwa waandishi wa habari ilibainika bado haviwapiki waandishi wa habari wakaiva inavyotakiwa kwa kuwa wanapokwenda kwenye vyombo vya habari wanashindwa kuhamisha walichosoma kwenye vitendo, huku wadau wakiomba hatua zaidi kutatua tatizo hilo.
Pia, imebaini kuwa waandishi wa habari hawaandiki kwa kina baadhi ya habari kama sakata la DP World (Mwekezaji katika Mamlaka ya Bandari Tanzania), vyama vya upinzani kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kuhamishwa kwa wananchi katika Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA).
Matokeo ya utafiti kwa upande wa Zanzibar, walaji wa habari wanapendelea zaidi habari zilizopo kwenye dijitali huku vyombo vya habari kama magazeti, TV na redio huku vikionyesha kutegemeana jambo ambalo linaonyesha kuwa dijitali sio tishio kwa uendelevu na ukuaji wa vyombo vilivyokuwapo.
Aidha, wadau wanaamini kuwa vyombo vya habari kama magazeti, TV na redio, ni muhimu kwa watu hasa kizazi cha zamani na kwamba ni muhimu vikatafuta kutumia fursa ya ujio wa mitandao ya kijamii.
Pia, ripoti hiyo ilibaini kuwa vyombo vya habari visiwani Zanzibar vinatoa huduma zaidi kuliko biashara kwa kuwa wanashindwa kupata fedha za kutosha kutokana na kukosekana watangazaji wakubwa.
“Mtangazaji mkubwa ni serikali ambao hatangazi kwenye vyombo vya habari binafsi, hali inayosababisha vingi kushindwa kumudu gharama za uendeshaji na hivyo kujiendesha kwa shida,” alisema.
Kwa upande wa sera, sheria na kanuni, wadau wanaona kuna ukandamizwaji na nyingine zimepitwa na wakati na zinatakiwa mpya ambazo zitakuwa rafiki kwa utendaji wa vyombo vya habari.
Ripoti hiyo imerejelea kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ambaye Machi 2022, aliagiza sheria zote za vyombo vya habari kubadilishwa, ili kujenga mazingira salama kwa waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma.
Aidha, akijibu jambo hilo Machi 2023, Waziri wa Habari Zanzibar, Tabia Mwita Maulid, alisema wako kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya Huduma za Habari ambayo imefikia asilimia 80 kwa wakati huo.
“Ingawa hadi wakati tunakamilisha sehemu ya kwanza ya ripoti hii mwaka huu, muswada ulikuwa haujafikishwa Baraza la Wawakilishi licha ya jitihada za uragibishi uliofanywa na wadau ambao umechukua muhongo mmoja,” alisema.
Kwa upande wa jinsia na maudhui, ripoti hiyo imebaini kuwa Zanzibar imekuwa kikwazo kwa muda mrefu kwenye sekta ya habari, na kwamba kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wadau mbalimbali huku waandishi wa habari wanawake wataendelea kuwa kwa wakati mgumu kuvunja mizizi iliyopo.
“Katika mazingira ambayo waandishi wa habari wanawake Zanzibar wametokana na mfumo dume uliopo kwenye visiwa hivyo, kukata mizizi hii ni muhimu sana, waandishi wa habari wanawake wataendelea kuongezeka kwa idadi, lakini kuna ukandamizaji na kuachwa nyuma,” alisema.
Kuhusu msaada wa kuendeleza vyombo vya habari, ripoti hiyo imebaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinapokea msaada wa fedha na rasilimali nyingine kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kuendeleza wafanyakazi wao na taasisi zao katika programu za miaka miwili.
“Msaada wa raslimali ni vifaa wa kazi kama laptop, ipads, rekoda, viyoyozi na vifaa vya kurusha matangazo, msaada wa kifedha umesaidia waandishi kupata mafunzo na utafiti licha ya kwamba hakuna matokeo makubwa,” inaainisha ripoti hiyo.
Kuhusu dijitali, waandishi wa habari wamekuwa tegemezi kwenye mitandao ya kijamii kujipatia taarifa huku wadau wakitaka kutumika kwa mitandao hiyo kutengeneza maudhui nzuri itakayowezesha kupata fedha kutoka facebook, YouTube na x (zamani Tweeter).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED