Wakazi wa Barabara ya Mtaa Lindi Kariakoo Kata ya Gerezani wilayani Ilala wamemlilia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa adha kubwa wanayoipata ya majitaka yaliyotuama kwa muda mrefu eneo hilo.
Wakazi hao wamesema wameingiwa na hofu kubwa ya kupata maradhi sugu ya mlipuko kufuatia kadhia hiyo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameagiza DAWASA, TARURA na DART kukutana mara moja kuweka maazimio ya pamoja kuondoa changamoto hiyo.
RC Chalamila amewataka DAWASA kupeleka magari kesho kushughulikia mfumo wa majitaka ambao wao ndio chanzo ya kero hiyo inayosababishwa na mfumò wa majitaka.
Pamoja na hayo amezitaka taasisi hizo kuacha janjajanja (usanii) kuacha migogoro yao ya kikazi na waongee lugha moja ili wamalize kero hiyo.
Akizungumza na Nipashe Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Gerezani Magharibi Mohamed Abd amesema kero hiyo inasabanishwa na mtaro mkuu uliopita mtaa wa Kipata unaopeleka maji baharini kuziba mbapo wahusika wa kutatua hilo ni DAWASA.
Wakati huo Chalamila akiwa katika ziara yake na ukaguzi wa miradi Ilala ametoa katazo la uoshaji magari pembezoni mwa barabara ambazo zimetengenezwa kwa fedha nyingi na kumuagiza Mkurugenzi wa Jiji waandalie maeneo mengine ya kufanya shughuli hizo ili mapato yaìngie serikalini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED