MTANDAO wa Wanaharakati wanaopinga usafirishaji haramu wa binadamu (TANAHUT), umetaja mikoa inayoongoza kwa biashara hiyo huku visiwa vya Zanzibar na Dar es Salaam, ikiongoza.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU) ili kuwajengea uelewa, Mkurugenzi Mtendaji wa TANAHUT, Wakili Edwin Mugambila, alitaja mikoa mingine ni Singida, Tabora, Shinyanga, Geita, Mwanza, Iringa, Manyara, Tanga, Mtwara, Arusha, Songwe, Mbeya, Kagera na Kilimanjaro.
Alisema visiwa vya Zanzibar ni lango kuu wakati Dar es Salaam ni mji wenye kazi nyingi za kutumikisha mabinti na watoto hasa biashara haramu ya ngono.
“Zanzibar ni lango kuu na Dar es Salaam ndio kitovu chenyewe. Dar es Salaam kuna biashara ya ngono inaendelea, kuna viwanda, uvuvi na biashara kubwa ya ngono na ndio maana unaona kuna massage spa na madanguro kila mahali,” alisema.
Alisema kwenye vituo vya mabasi, mtandao huo unashuhudia utumikishwaji wa watoto kwenye biashara ndogo ndogo na kwamba wengine kwenye viwanda, migahawa na hoteli.
Mikoa ya Geita, Shinyanga na Tabora, alisema kuna utumikishwaji wa watoto kwenye mashamba makubwa ya tumbaku na migodini, ambako pia kuna biashara haramu ya ngono.
Aidha, alisema kwenye baadhi ya mikoa, watoto wa kike na wa kiume pamoja na mabinti, wanarubuniwa na kusafirishwa kwenda kwenye miji mikubwa kwa ahadi ya kazi halali, lakini wanaishia kutumikishwa kwenye ngono.
Mugambila alisema ili kukabiliana na usafirishaji haramu, TANAHUT inatumia mbinu ya kuzuia, kuwalinda waathirika na kuwashitaki wahusika.
Aliitaka jamii iungane kupinga biashara hiyo ili Tanzania iwe sehemu salama kwa ustawi wa watu wote.
Mkurugenzi wa Programu wa TANAHUT, Jones John, alisema tatizo hilo linahitaji nguvu za pamoja kulikabili.
Alitoa rai kwa wanafunzi wanaochukua Shahada za Uzamili na Uzamivu, kufanya utafiti na kutoa maandiko ya kitaaluma, yatakayosaidia taifa kuondokana na tatizo hilo, linaloathiri zaidi wanawake na watoto.
“Tunashirikisha walimu na wanafunzi ili kwa pamoja waone kuna uwezekano gani kuingiza tatizo hili kwenye masomo yao ili kuchechemua hamasa ya wanafunzi na jamii nzima kufahamu tatizo hili,” alisema.
John alisema lengo la wanaharakati kushirikiana na vyuo ni kutengeneza kizazi cha wadau wengi wenye uelewa ambao wanaweza kutumia elimu yao kulitafutia ufumbuzi.
Mkurugenzi wa Nyumba Salama (Courage Worldwide), Suzan Shoo, alisema waathirika wakubwa wa biashara hiyo ni wanawake na watoto, kutokana na kwamba ni makundi yasiyo na sauti wala nguvu ya kujitetea.
“Usafirishaji haramu wa binadamu unatokea kwenye jamii yetu. Wengi wanadhani unatokea nje ya nchi kumbe unatokea mitaani na kwenye vijiji vyetu. Tunahitaji nguvu ya pamoja kulikabili,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED