Waziri Ndumbaro awapa elimu ya uraia wananchi wa Kibirizi, Kigoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:04 PM Jan 25 2025
Waziri Ndumbaro awapa elimu ya uraia wananchi wa Kibirizi, Kigoma
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Ndumbaro awapa elimu ya uraia wananchi wa Kibirizi, Kigoma

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro na Timu ya wataalamu wa msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) wamepiga kambi leo katika Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma mkoani Kigoma kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria na elimu ya uraia kwa wananchi wa eneo hilo.

Katika kampeni hiyo ambayo imeanza juzi mkoani humo na inalenga kuvifikia vijiji 240 mkoani humo, Waziri Ndumbaro  amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza wananchi wapewe elimu hiyo sambamba na elimu ya sheria na Katiba, Haki za binadamu na msaada wa kisheria ili wajue sheria na kutokiuka sheria.

“Tanzania ni nchi nzuri yenye kuvutia wema na wabaya, yenye neema kedekede sisi tumejaa neema, ina amani na utulivu na mfumo mzuri wa maisha, kuna nchi hazina haya tuliyo nayo sisi, uzuri huu unawavutia wengi wengine wanakuja kwa kufuata taratibu rasmi za uhamiaji, wapo wanaokuja kwa njia za panya hawa ndio wanaotuponza,”amesema.

Amesema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuwa makini kwa kuwa tatizo la mipakani kuna kuingiliana kwa makabila na nchi jirani.


Awali, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda amesema ni maono ya Rais Samia wananchi wapate nafasi ya kusikilizwa na wapewe msaada wa kisheria kwenye changamoto zao.

Amesema pamoja na matatizo mengine ya kisheria yaliyopo Kigoma Mjini kuna suala la utata wa uraia wa watu.