Simba: Tutacheza kama fainali leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:30 AM Jan 26 2025
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola
Picha: Mtandao
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola

KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema wataingia kwenye mchezo wa raundi ya tatu, Kombe la FA dhidi ya Kilimanjaro Wonders kucheza kama fainali, kwani hawataki yawatokee kama ilivyokuwa kwa Mashujaa FC, na Green Worriors miaka kadhaa nyuma.

Akizungumza kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mkoa Kilimanjaro, Matola alisema hawawezi kusahau kile kilichowatokea miaka ya nyuma hivyo wataingia kamili kwenye mchezo huo.

"Tumejipanga vizuri na mchezo huu kwa sababu ni mechi ya mtoano, siku zote aina hizi za mechi zimekuwa hazina mwenyewe, ukikosea tu uko nje ya mashindano, kutokana na hilo tunauchukua huu mchezo kwa umuhimu mkubwa.

Tunakwenda kucheza mechi hii kama tunakwenda kucheza fainali kwa sababu tuna uzoefu na mashindano haya, tena na timu kama hizi zimeshawahi kututoa si mara moja kwa hiyo tunaichukulia kwa umuhimu mechi ya kesho, tunakwenda kucheza kama ni mchezo wa mwisho wa fainali."

Simba iliwahi kutolewa kwenye hatua za mwanzo, Desemba 22, 2017, dhidi ya Green Warriors kwa penalti 4-3, baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kujirudia Desemba 26 kwenye uwanja huo huo wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilipotolewa kwenye raundi ya tatu kwa mabao 3-2, dhidi ya Mashujaa FC, iliyokuwa Ligi Draja la Kwanza wakati huo.

Mashabiki wa Simba leo wanatarajiwa kumimimika kwa wingi, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, uliopo maeneo ya Mwenge saa 10:00 jioni kuona timu yao baada ya kuzuiwa, Jumapili iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa makundi Kombe la Shirikisho, dhidi ya CS Constantine ya Algeria baada ya kufungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kufuatia vurugu zilizojitokea kwenye mchezo wao dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia uliochezwa kwenye uwanja huo huo, Desemba 15 mwaka jana.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Wonders, Daud Macha 'Ndailagije', alisema wataingia uwanjani kwa ajili ya kupambana na timu kubwa, nzuri ya Simba kwa kuiheshimu.

 "Tumekuja kwa ajili ya kupambana kwenye mchezo huu, kikosi kipo vizuri, staili yetu ya kucheza ni ya kawaida tu, tunaiheshimu Simba kwa sababu ni timu kubwa.

Hatutarajii makubwa sana kwenye mchezo huu, lakini huu ni mchezo wa mpira, hatuwezi kusema tumekuja kwa ajili ya kushindwa, tumekuja kwa ajili ya kujifunza na kupambana pia," alisema.

Msimu uliopita, Simba ilitolewa katika hatua ya 16 bora dhidi ya Mashujaa FC kwa penalti 6-5, mechi ikichezwa, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 kwa kufungana bao 1-1.