JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu wawili, akiwamo wakili wa kujitegemea, kuhusiana na taarifa zilizosambaa katika mtandao wa kijamii zinazoeleza kunusurika kuuawa, kutekwa na kupigwa nyundo kichwani raia wa Afrika Kusini, Suzan Shawe (75).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, katika taarifa yake jana, aliwataja watuhumiwa hao ni Qamara Valerian (36) ambaye ni Wakili wa Kujitegemea na Benjamin Paul (19) dereva pikipiki (bodaboda).
“Raia huyu wa kigeni alivamiwa nyumbani kwake eneo na Njiro, Block C1, Januari 21, mwaka huu, saa 3:00 asubuhi na watu waliotumwa na Valerian kwa nia ya kumtoa kwa nguvu kwa madai ya kutolipa kodi ya nyumba hiyo anayoishi,” alisema.
Kamanda Masejo alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya upelelezi kukamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kufuata sheria na kanuni katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
Kadhalika, alitoa rai kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Arusha kufanya uchunguzi wa taarifa zao na kujiridhisha kabla ya kuzitoa ili kuondoa taharuki kwa wananchi na wageni wanaofika katika mkoa huo.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Njiro, Susan alidai saa 3:00 asubuhi akiwa hapo walifika watu asiowafahamu wakiwa na pikipiki sita walizokuwa wamepakizana watatu watatu na kuvamia nyumba hiyo ambayo amepangisha na ameishi hapo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Alisema watu hao walikuwa na kiongozi wao waliokuwa wakimwita kwa jina moja la Abdul ambaye alikuwa akiwashurutisha wenzake kumtoa ndani ya nyumba hiyo kwa nguvu.
“Nilikuwa chumbani kwangu nikasikia kelele, msichana wangu anayenisaidia kazi za nyumbani alikuja na kuniambia kuna tatizo kubwa nje. Nilipofunga mlango wangu kwa komeo na baada ya muda mfupi nilisikia mlango ukivunjwa na watu hao wakiongozwa na Abdul wakaingia chumbani,” alisema.
Alisema walipoingia walimkamata na kumpeleka bafuni kisha wakaanza kumpiga, huku mmoja alimpiga kwa nyundo kichwani.
Alidai kuwa walimvua nguo na kumburuza kutoka ghorofani hadi getini akiwa utupu, wakimsisitiza atoke ndani ya nyumba hiyo kwa sababu anadaiwa kodi.
“Nipo hapa nchini kwa ajili ya kufuatilia mirathi ya marehemu wangu aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita na tumeishi naye hapa kwa zaidi ya miaka 20 tukiwa wapangaji na tumepangishiwa nyumba hii na Irene Sianga anayeishi nchini Uingereza.
“Tumepangishwa kwa makubaliano ya kumlipa kiasi cha Dola za Kimarekani 800 na nimekuwa nikilipa kila mwezi na nimemlipa fedha mwanzoni mwa mwezi huu,” alisema.
Alidai wakati wanaendelea kumshurutisha atoke kwenye nyumba hiyo, baadhi ya watu walibaki chumbani kwake wakipekua na kuchukua vitu mbalimbali zikiwemo fedha.
Mfanyakazi wa Suzan, Ayubu Malolo, alisema wakati akiendelea na majukumu yake nyumbani hapo lilifika kundi la watu wakiwa wamepakizana kwenye bodaboda wakiwa na mapanga na nyundo na kumwuliza sababu za kuishi katika nyumba hiyo bila kodi.
“Kabla sijawajibu walinitaka niwapeleke kwenye chumba cha bosi wangu huku kiongozi wao aitwaye Abdul akitangulia na kwenda kuwafungia mbwa kwenye banda kwa komeo waliokuwa wakipiga kelele,” alidai.
Mfanyakazi huyo alidai alipowafikisha ghorofani na kuwaonesha chumba cha bosi wake walimweka chini ya ulinzi na kisha wakavunja mlango wake na kuingia chumbani kwake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED