MTOTO anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili ambaye jina lake halijafahamika, amekutwa katika msitu wa Mkweni ulioko kati ya mkoani Shinyanga na Geita, akiwa amedhoofika mwili.
Amekutwa na wasamaria wema na tayari amekabidhiwa katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima Zaqahana kilichoko Mji mdogo wa Kagongwa, Manispaa ya Kahama.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Zakia Mwambiko, alisema walimpokea kutoka kwa maofisa ustawi wa jamii waliodai kuwa ameokotwa na watumishi wa Halmashauri ya Ushetu akiwa amelazwa kando ya barabara ya pori hilo.
Zakia alisema mtoto huyo amempatia jina moja la Bahati na kuwa kwa sasa hawezi kula zaidi ya kunywa maji na maziwa, hali iliyosababisha kuumwa mara kwa mara.
“Majibu ya daktari ni kuwa viungo vyake vina shida hali inayosababisha miguu kukosa nguvu ya kukanyaga chini ya ardhi. Shingo yake haitulii au kusimama kama watoto wengine. Haongei, ana uoni hafifu hali inayomsababishia kushindwa kulala na pia kupata choo,” alisema.
Aliwaomba wadau kwa kushirikiana na serikali kuangalia namna ya kumpeleka mtoto huyo katika hospitali kubwa zenye madaktari bingwa kuchunguza afya yake.
Mkurugenzi wa The Little Ones Charity Plus Foundation, Mhandisi Manyango Barnabas, alisema kitendo alichofanyiwa mtoto huyo ni ukatili ambao haupaswi kuvumilika ndani ya jamii.
Barnabas aliunga mkono kazi kubwa inayofanywa na kituo hicho kwa kutoa msaada wa mafuta ya kula, mchele, maharage, sabuni, madaftari, dawa za meno na miswaki, mahindi, unga wa sembe na ngano.
Mkazi wa Kagongwa, Jane Haule, alisema ugumu wa maisha katika familia unasababisha baadhi ya wazazi kuzikimbia familia zao na wakati mwingine baba kukataa ujauzito au mtoto kukataliwa anapozaliwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED