Pamba: Unyonge mwisho mzunguko wa kwanza tu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:43 AM Jan 26 2025
Timu ya Pamba Jiji
Picha: Mtandao
Timu ya Pamba Jiji

KLABU ya Pamba Jiji, imeeleza kufurahishwa na usajili ilioufanya kwenye dirisha dogo la uhamisho lililofungwa Januari 15 mwaka huu huku ikiwa na matumaini ya kufanya vyema mechi zijazo na kuja na kauri mbiu ya 'unyonge mwisho mzunguko wa kwanza.'

Ofisa Habari na Klabu hiyo, Moses William, amesema jana kuwa wameridhishwa na usajili walioufanya kwa kuongeza wachezaji bora ambao wataleta ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza, Februari Mosi.

Pamba inatarajiwa kucheza mechi ya raundi ya 17, Februari 5 mwaka huu dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Kikosi hicho tayari kimeshaingia kambini kujiandaa na mchezo huo pamoja na mechi zinazofuata za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

"Mechi dhidi ya Dodoma Jiji, haItokuwa mechi rahisi, haitokuwa mechi ya kizembe, lakini sisi kama Pamba Jiji tumejindaa vizuri kwenda kutoa burudani. Tunasema hivi, kwa usajili huu ambao tumeufanya kwenye dirisha dogo, ukiunganisha na kazi inayofanywa na benchi la ufundi, tunasema hivi.., unyonge mwisho mzunguko wa kwanza," alisema.

Pamba jiji imesajili wachezaji 11 kwenye dirisha dogo, kuelekea mechi za mzunguko wa pili, ambao ni Deus Kaseke, Habib Kyombo, Hamad Majimengi, Cherif Ibrahim kutoka Cameroon, na Zabona Mayombya.

Wengine ni kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burundi, Shassir Nahimana aliyesajiliwa kutoka Tuskera ya Kenya ambako alikuwa nahodha, kipa raia wa Sierra Leone, Mohamed Kamara, straika Mcameroon,  Francois Bakari, Mathew Tegis kutoka Shabana ya Kenya, kiungo mshambuliaji kutoka Guinea, Abdulaye Camara na beki wa kati Mgambia, Modou Camara.