Barrick kusaidia kuinua michezo

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:37 AM Jan 26 2025
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Victor Lule
Picha: Mtandao
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Victor Lule

KAMPUNI ya uchimbaji dhahabu ya Barrick imepanga kusaidia ukuaji wa michezo katika maeneo yanayozunguka migodi yake ya North Mara mkoani Mara na Bulyanhulu mkoani Shinyanga.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa ripoti ya kampuni hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Victor Lule, alisema wamepanga kuhangia ukuaji wa michezo kuanzia ngazi ya chini na kwa sasa wapo kwenye mchakato wa ndani kuanza programu hiyo.

“Tayari tumeanza huu mchakato, tunataka kuinua michezo kuanzia ngazi ya chini kabisa, tunafahamu michezo inaleta ushirikiano na mahusiano mazuri, tunajipanga kufanya hivyo,” alisema Lule.

Lule alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa ni namna gani kampuni hiyo inasaidia kwenye sekta ya michezo.

Awali, mbunge wa jimbo la Msalala, Iddi Kassim, aliomba kampuni hiyo kuisaidia timu ya Bulyanhulu ‘Buly FC’ inayoshiriki ligi za chini ili iweze kupanda mpaka ngazi za juu.

“Tunafahamu kuna mkakati wa vijiji 16 katika kuendeleza michezo, lakini niombe pia tuna timu yetu ya eneo hili, tunaomba ipewe udhamini ili iweze kufanya vizuri, na hii timu imebeba jina la mgodi,” alisema Iddi.

Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema wataangalia namna bora ya kusaidia michezo katika maeneo yanayozunguka migodi ya kampuni hiyo ikiwa pamoja na kutengeneza miundombinu.