Atolewa uvimbe kilo 1.4 katika kizazi, aliishi nao miaka mitano

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:31 AM Jul 23 2024
Mfumo wa uzazi.
Picha: Mtandao
Mfumo wa uzazi.

MAMA wa watoto wanne, mkazi wa Siha, mkoani Kilimanjaro (jina tunalo), ametolewa uvimbe wenye uzito wa kilogramu 1.4 katika kizazi ambao ameishi nao kwa zaidi ya miaka mitano.

Uvimbe huo kitaalamu unaitwa ‘mayoma' ulikuwa unaendelea kuota katika kizazi, huku ikielezwa ulikuwa na uwezekano wa kutokea ndani ya mfuko wa uzazi au pembeni mwa ukuta wa kizazi.

Akizungumzia upasuaji huo uliofanywa na jopo la madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Siha (DMO), Dk. Paschal Mbotta, alisema upasuaji huo uliochukua saa mbili na nusu, ulilenga zaidi kumwepusha mama huyo (44) na maumivu makali aliyokuwa akiyapata pamoja na kumwepusha kupata saratani ya kizazi.

"Tulikuwa na kambi ya siku tano ya madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, ambayo tuliifanya kwa kutumia mapato ya ndani ya hospitali yetu ya Wilaya ya Siha.

"Sasa huyo mama alikuja tukamfanyia vipimo akaonekana ana tatizo la uvimbe katika kizazi. Alikuwa na upungufu wa damu, tukamwongeza damu na baada ya siku chache tukaingia naye katika operesheni.

"Sasa tulipoingia katika operesheni, tukakuta kitu kingine na tulichokiona kwenye vipimo vyetu. Ule uvimbe ulikuwa umekula kizazi chote na badala ya kuondoa hiyo mayoma peke yake ilibidi tuondoe kizazi chote; kwa sababu ilikuwa ni ngumu kutenganisha ule uvimbe na kizazi," alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Mbotta, mama huyo hivi sasa anaendelea vizuri kiafya, Hospitali ya Wilaya ya Siha ikitoa huduma hizo za kibingwa kwa wananchi wake pamoja na wilaya jirani kuanzia Julai 15 hadi Julai 19 mwaka huu.

Kambi hiyo ilihusisha madaktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya kinamama (gynacologist) kutoka Hospitali Teule ya St. Joseph (Moshi), ikiongozwa na Dk. James Kimario na Dk. Peter Samweli kutoka Hospitali ya Faraja.

Dk. Mbotta alisema hakuna sababu maalum za kitaalamu zinazousababisha uvimbe huo, lakini tatizo kama hilo linatokea kutokana na historia ya familia, uzito mkubwa na wale wasiozaa (wagumba) au wanaotumia dawa za vichocheo.