Askofu Shoo aibuka na rushwa ya aibu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:34 AM May 27 2024
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikirsto Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo.
Picha: Maktaba
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikirsto Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Kikirsto Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo ameutaja ubinafsi ni sumu mbaya iliyofikisha baadhi ya watu kwenye hatua ya kutaka fedha chafu ili kupata madaraka na kujinufaisha kwa ustawi wao wenyewe badala ya maslahi ya taifa.

Amesema kwa kuendekeza ubinafsi taifa linafunga baraka zake zilizoahidiwa na Mungu, akitaka Watanzania kutumia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani kupata viongozi wanaojali maslahi ya wengi badala ya maslahi binafsi na familia yake.

Dk. Shoo ambaye Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini alitoa kauli hiyo jana wakati wa Ibada ya Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya CCT yaliyofanyika mkoani Mtwara.

Alisema ubinafsi umesambaratisha familia na kuleta madhara makubwa, ndani ya kanisa au usharika watu wanakusanyika lakini hakuna umoja ndani yao.

"Mafarakano ndani ya kanisa ni matokeo ya ubinafsi uliopitiliza na kutosimama na Mungu, unaharibu ustawi, mshikamano kwenye jamii ya watu kwa kuwa tunu ya Tanzania ni kutunza umoja. Inaamka roho ya kugawa watu kiukanda, ukabila ujue ibilisi ameingia na kupata nguvu.

"Ndani ya vyama vya siasa kuna migongano mikubwa kiasi kwamba wengi hawajui mwelekeo ni wapi, tatizo ni ubinafsi, kila mtu anaangalia mambo yake na si ustawi wa kundi, nchi na vizazi vyake. Tuko pamoja kama kanisa ila kuna viongozi wameacha roho ya utumishi na kuangalia maslahi yao…'mungu pesa’ ndiye amekuwa mungu wao badala ya kutumikia na kulisha kondoo wa Mungu na kusimama katika ukweli wa neno.

"Hata kutumia njia za vitisho, udanganyifu ili kuwatisha watu watoe sadaka. Wanaojiita watumishi wa Mungu warudi katika wito wafanye kwa uaminifu. Si kujifanya mabwana au kutaka fedha ya aibu ili kupata madaraka fulani… tuwe na umoja, kusiwe na sauti mbili," alisema.

Alihimiza Watanzania kulipenda taifa na kuacha kujifikiria binafsi bali kuangalia ustawi wa nchi, kuona "tunataka Tanzania ya namna gani miaka 100 ijayo baada ya waliopo kuondoka?" 

Askofu Dk. Shoo alieleza, "Viongozi wabinafsi tulionao ambao wanataka Tanzania iwe mali yao, chochote kinachopatikana ni kwa ajili yao na familia yao, 'kina hohehahe watajijua', ubinafsi ni sumu mbaya sana, tunaondoa baraka zilizoahidiwa kwa Tanzania."

Alisema mustakabali wa nchi unategemea umechagua kiongozi wa aina gani kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, na ni wajibu wa kila Mtanzania kuangalia ni viongozi gani waadilifu na wacha Mungu na wenye kuipenda Tanzania na watoto wa Tanzania.

"Viongozi waadilifu, wacha Mungu hawa ndio tuwasukume, tuwachochee wagombee…ndivyo viongozi wazuri wanaofaa nchi wanavyopatikana. Usiangalie dini, madhehebu yao pale, kijijini unamfahamu, watu wema wanafahamika, hadi wilayani wanafahamika, watu hawa ndio tukawaweke na kuwapa madaraka ya kuongoza nchi.

"Tukalifanye kwa pamoja maana ni wajibu wetu, uamuzi mwingi unafanyika kwenye wilaya, halmashauri tukiwa na viongozi wabaya tunaishia kulalamika.

"Kwenye Uchaguzi Mkuu tunachagua wabunge ambao ndio wawakilishi wetu, unachagua mtu ambaye akishakanyaga lile jengo hajali alikotokea wala mahangaiko ya waliomchangua. Makosa ni ya nani? Ni wewe (mpigakura) uliyemchagua, tuchague ambaye atajali matakwa, maslahi ya anaowawakilisha bungeni. Maslahi ya taifa, tuache kukubali hongo," alisisitiza.

Askofu Shoo alisema kuna shida kubwa ya rushwa kwenye uchaguzi na kwamba ni mambo ambayo anatamani kusimama pamoja na watu wema bila kujadili dini, madhehebu kukataa rushwa katika uchaguzi wa mwaka huu na mwakani.

"Tukatae hata kama kuna mbunge amekuwakilisha sasa (miaka mitano) umeona ameweka maslahi ya waliomtuma (wananchi) mchague tena, lakini kama aliwasahau tangu 2020 anarudi mwaka huu na ujao akipita kwenye kila nyumba, mwambie 'sikujui kama ambavyo wewe hukunijua," alisema.

Askofu Shoo alisema wananchi walitoa maoni kuhusu Katiba Mpya, sheria za vyama vya siasa na zingine zinazohusu uchaguzi, lakini hajui ni kwa kiasi gani maoni yao, yakiwamo ya viongozi wa dini, yamezingatiwa.

“Ombi langu na wito wangu na sisi tunaopenda nchi yetu, kwa sauti ya pamoja tuseme viongozi madaraka na mamlaka, wabunge tuliowachagua mtuwakilishe, sikilizeni maoni yetu, heshimuni maoni yetu na myafanyie kazi. Kwa umoja tukipiga kelele kwa pamoja wataheshimu na kutekeleza," alisema na kuonya kuwa pasipo umoja hakuna amani, hakuna baraka kwa familia, kanisa na nchi.

KINANA ALONGA

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana naye ametaja sifa za kiongozi wanayemtaka ndani ya chama hicho kuwa ni anayekubalika kwa jamii, anayejituma, asiyetoa rushwa fedha na asiye na longolongo. 

Aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, akisisitiza wabunge kuhakikisha wanaonekana majimboni. Wananchi wafunge milango kwa mbunge ambaye haonekani katika eneo lake la kazi. Ni kama ilivyo rai ya Askofu Dk. Shoo. 

"Ukumbuke kwamba kabla ya kuja kuwa mheshimiwa kuna wengine walikuwa waheshimiwa, jambo lingine mbunge usiulizwe huyu tangu awe mbunge amefanya nini, kuwe na maendeleo yanayoonekana," alisema Kinana. 

Alisema kuwa mambo yanayofanya CCM iendelee kudumu ni demokrasia ndani ya chama, akieleza kuwa siku wakivunja utaratibu huo ndani ya chama hali yao itakuwa mbaya. 

"Wanachama wa CCM hakikisheni mnajua miradi yote ya maendeleo inayofanyika katika maeneo yenu ili ikifika wakati wa uchaguzi, msifanye kazi ya kukejeli na kutukana, hiyo si desturi ya chama chetu, kazi yetu ni kusimamia ilani ya CCM.

*Taarifa za ziada na Maulid Mmbaga