Afisa elimu Singida na wenzake wanne waingia matatani

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 01:19 PM Jul 26 2024

AFISA Elimu Mkoa wa Singida,Dk.Elipidius Baganda.
Picha: Mpigapicha Wetu
AFISA Elimu Mkoa wa Singida,Dk.Elipidius Baganda.

AFISA Elimu Mkoa wa Singida,Dk.Elipidius Baganda na maafisa wengine watano wa Idara ya Elimu mkoa na Manispaa ya Singida wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na kughushi nyaraka na kujipatia mamilioni ya fedha.

Maafisa hao mbali na Dk. Baganda ,wengine ni Afisa Michezo Mkoa wa Singida, Amani Mwaipaja, Afisa Elimu ya Watu Wazima Manispaa ya Singida, Siah Mtafya, Afisa Elimu maalum Manispaa ya Singida, Deonatus Malima na Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi Manispaa ya Singida, Shehe Mwakilambe Khoja.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Sipha Mwanjala, amesema hayo leo (Julai 26,2024)  wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Aprili hadi Juni baada ya waandishi kumuuliza kwamba kuna tetesi za maafisa wa Idara ya Elimu Mkoa wiki iliyopita waliwekwa mahabusu kwa kosa ambalo halijawekwa wazi.

"Ni kweli wapo watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida  ambao wamefikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika,wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mamlaka na kughushi nyaraka," alisema.