ACT- Wazalendo: Wanachama milioni 10 kwa miezi 10 ni silaha yetu ya ushindi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 AM Jul 23 2024
Kiongozi wa Chama Dorothy Semu.
Picha: ACT
Kiongozi wa Chama Dorothy Semu.

Chama cha ACT Wazalendo kimeanza awamu ya kwanza ya kampeni ya kusajili wanachama milioni 10 katika kipindi cha miezi 10 kinachoanza Julai 2024 mpaka April 2025.

Awamu hiyo itafikia mikoa 22 yenye majimbo 125 kati ya majimbo yote 214 ya Tanzania Bara. Akielezea lengo la Kampeni hiyo Kiongozi wa Chama Dorothy Semu, akiwa Jimbo la Mvumi mkoani Dodoma amesema;

“Tumeamua kuendesha kampeni ya kusajili wanachama katika mfumo wa kisasa wa ACT Kiganjani kwasababu tumedhamiria kushiriki na kushinda chaguzi ili kuongoza Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji pamoja na kushika dola 2025.’’ amesema na kuongeza kuwa; 

"Mwezi Septemba chama chetu kitafanya awamu ya pili ya kampeni ambayo itamalizia majimbo 89 yaliyobakia ili kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ACT Wazalendo tutakuwa tumefikia majimbo yote 214 ya Tanzania Bara.Wanachama wa chama cha siasa ndio mtaji wa kwanza wa chama." amesema Dorothy

Ameongeza kuwa wanachama pamoja na watanzania wengine wakitupigia kura tutaongoza Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa kuonesha namna boresha ya kuendesha vijiji vyetu, mitaa na vitongoji vyetu kwa maslahi ya wananchi wote.

"Watanzania wanataka mabadiliko, wamekuwa wakiumizwa na gharama kubwa za maisha na umaskini, ukosefu wa ajira, fursa na huduma mbovu za jamii.

Kiongozi wa Chama Dorothy Semu.

Amesema wananchi wanataka kuona wanamudu maisha yao kwa kuweza kugharamia mahitaji yao ya msingi, kupata fursa ya ajira, kazi na kufanya shughuli za kujipatia kipato bila bughudha na vikwazo.

Ameongeza kuwa: "ACT Wazalendo katika kampeni hii imelenga kuwaunganisha Watanzania kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote. Taifa ambalo Serikali itahakikisha sera za uchumi zinapunguza gharama za maisha ya wananchi wote, itahakikisha kuwa uchumi unakua na kuzalisha ajira nyingi na kila Mtaznania anapata matibabu kwa kuunganishwa kwenye mfumo wa hifadhi ya Jamii (NSSF na PSSSF)"

Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita amesema umuhimu wa wananchi kujisajili kuwa wanachama wa ACT Wazalendo ni kutuma ujumbe kwa CCM kuwa wananchi wamewakataa na wajiandae kuondoka madarakani kwenye chaguzi zijazo.

Amesema wananchi wanapaswa kujiunga na vuguvugu hili kwa ajili ya kuikomboa nchi kutoka katika mikono ya Chama tawala.

Aidha, Mchinjita ameongeza kuwa nguvu ya wananchi kuiwajibisha Serikali ipo mikononi mwao, kwa kuhakikisha wanaungana katika chombo chenye shabaha hizo. Ndio maana leo tumeanza kampeni hii ya kuwaunganisha watanzania. Kila ulipo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jiunge na ACT Wazalendo. Chama cheye dhamira ya kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka.