Zaidi ya watu 50,000 wakimbia Haiti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:34 AM Apr 03 2024
Polisi washika doria mjini Port-au-Prince nchini Haiti.
Picha: Odelyn Joseph/AP/dpa/picture alliance
Polisi washika doria mjini Port-au-Prince nchini Haiti.

Zaidi ya watu 53,000 wamekimbia mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince katika wiki tatu za mwezi Machi kufuatia vurugu za magenge yenye silaha ziliposababisha uharibifu mkubwa kwa raia.

Makadirio ya Umoja wa Mataifa yaliotolewa jana, yanaonesha kuwa maelfu ya watu waliondoka mjini Port-au-Prince kati ya Machi 8 na 27 huku ghasia zikizuka tena kipindi cha Pasaka na mwanzoni mwa mwezi Aprili.

DW imeripoti kuwa, Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema kuwa unyanyasaji wa haki za binadamu ulikuwa unafanyika katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono.

Mzozo huo pia umezuia kusafirishwa kwa bidhaa muhimu na misaada ya kibinadamu katika mji huo mkuu.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu wengi waliopoteza makazi wanasafiri kuelekea rasi ya Kusini ya nchi hiyo ambayo bado inajikwamua kutokana na tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2021.