Tume ya Ukimwi Z’bar yatengewa bil. 33.4/-

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:19 AM Sep 21 2024
Tume ya Ukimwi Z’bar yatengewa bil. 33.4/-
Picha:Mtandao
Tume ya Ukimwi Z’bar yatengewa bil. 33.4/-

JUMLA ya Sh. bilioni 33.4 zimetengwa na Serikali ya Zanzibar kwa ajili ya kuiwezesha Tume ya Ukimwi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kufuatilia makundi maalumu ikiwamo vijana kuona yanadhibitiwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman, alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani jana, aliyetaka kujua mikakati ya kupambana na Ukimwi kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi ikoje.

Suleiman alisema Tume hiyo imepewa majukumu mengi ikiwamo kuhakikisha maambukizi yanayotokana na ugonjwa huo yanapungua kwa kiasi kikubwa.

Aidha, aliitaja mikakati mengine ikiwamo kutoa elimu ya kupambana na Ukimwi kupitia makundi mbalimbali hatarishi ambayo yanaongoza kwa maambukizi mapya.

Akitoa takwimu, alisema maambukizi mapya yamepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia mwaka 2005 na ni mwaka ambao serikali ilianzisha huduma za matibabu kwa waathirika wa ugonjwa wa ugonjwa huo ikiwamo kuwapatia dawa kwa watu wanaoishi na VVU.

Alisema kwa miaka minne iliyopita maambukizi ya ugonjwa huo yamepungua kutoka watu 519 waliopata maambukizi mapya kwa mwaka 2020 hadi 362 kwa mwaka 2023.

Alisema kwa mwaka 2024 hadi kufikia Julai ni watu 213 ambao waligundulika na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ambao tayari wanatumia dawa za kufubaza maradhi hayo.

''Mheshimiwa Spika takwimu hizo zinaonesha kwamba idadi ya watu wanaopata maambukizi mapya mwaka hadi mwaka inaendelea kupungua ikiwamo wananchi wenyewe kuwa tayari kujitokeza kupima afya zao,” alisema.

Aliyapongeza mashirika ya kimataifa yanayopambana na ugonjwa wa Ukimwi kwa misaada yao mikubwa ambayo imesaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huo.

Aliyataja mashirika hayo ikiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ugonjwa wa Ukimwi (UNAIDS) pamoja na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR).