TRA yaeleza teknolojia ilivyopaisha ukusanyaji mapato ya robo mwaka

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 02:30 PM Oct 19 2024
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda.
Picha: Mtandao
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetaja sababu ya kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kwa robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha kuwa ni matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFDs) na Mfumo wa Stempu za Ushuru wa Bidhaa (ETS).

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni kutokana na usimamizi thabiti wa matumizi ya EFDs na ETS.
TRA ina jukumu la kukusanya Sh. trilioni 29.415 kwa mwaka ikiwa ni sehemu ya bajeti ya kitaifa ya Sh. trilioni 49.3. 

Ili kufikia lengo hili, mamlaka ilihitajika kukusanya wastani wa Sh. trilioni 2.45 kwa mwezi. 

Hata hivyo, katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa fedha, imekusanya Sh. trilioni 7.79, ikiwa na wastani wa Sh. trilioni 2.6 kwa mwezi, na kuvuka malengo ya kila mwezi.

Mwenda alisema mafanikio hayo yameboresha ufuatiliaji wa miamala na ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa zinazotozwa kodi. 

Alisema mifumo hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanafikia na kuvuka malengo ya mamlaka ya ukusanyaji wa mapato.
Mfumo wa EFDs unafuatilia miamala ya mauzo kwa biashara mbalimbali kuhakikisha kwamba, wanaripoti mapato yao kwa usahihi, hivyo kupunguza ukwepaji wa kodi.

Pia, mfumo wa ETS unafuatilia bidhaa zinazotozwa ushuru kama vile vinywaji, pombe na tumbaku, na kuhakikisha kodi inakusanywa ipasavyo.

Alisema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, TRA ilivuka malengo yake, ikifikia asilimia 104 ya lengo mwezi Julai na Agosti, huku mwezi Septemba ikiweka rekodi ya ukusanyaji wa Sh. trilioni 3.18, ambayo ni rekodi mpya ya mwezi mmoja.

Mwenda alisema sera za TRA zinazowatambua walipa kodi kama washirika, zimechangia katika kuboresha mazingira ya utii wa kodi. 

Kadhalika alisema TRA imeanzisha mipango kama ‘Alhamisi ya Mlipa Kodi,’ ambayo inawapa fursa walipa kodi kuwasilisha malalamiko yao na kupata suluhisho kwa wakati.

Alisema TRA imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa, ambao wamechangia asilimia 43 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa katika robo ya kwanza. 

Mwenda alisisitiza kuwa utangulizi na utekelezaji mzuri wa teknolojia hizo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukwepaji wa kodi na kuhakikisha uwazi zaidi katika michakato ya kodi. 

“Uboreshaji wa mapato ya Tanzania pia, unakuja sambamba na upaishwaji wa mkataba wa ETS na mtoa huduma SICPA, ambao mfumo wake wa kisasa wa ufuatiliaji wa kodi unasaidia TRA katika kuchukua hatua za utekelezaji,” alisema.

Pia alisema  sera nzuri zinazowachukulia walipakodi kama washirika, badala ya wapinzani, pia zimechangia mafanikio hayo.

Alisema TRA imeimarisha ushirikiano wake na wafanyabiashara, ikiwa ni pamoja na mipango kama ‘Alhamisi ya Mlipakodi,’ ambayo inawawezesha walipakodi kutoa malalamiko yao na kupata suluhisho kwa wakati.

"Tumejitoa kusikiliza wafanyabiashara na kuwaunga mkono ili waweze kufanikiwa. Hii, kwa upande mwingine, husaidia kupanua wigo wa walipa kodi," alisema.

 Aliwahimiza wafanyabiashara ambao bado hawatii sheria za kodi kujisajili na kuanza kuchangia sehemu yao, hasa wale wanaofanya kazi bila Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Aliwakumbusha wamiliki wa biashara kwamba, usajili wa TIN ni bure na aliwahimiza kuanza kulipa kodi.

"Tunatoa wito kwa wale wanaoendesha biashara ambazo hazijasajiliwa kujiunga na mfumo rasmi wa kodi na kuchangia maendeleo ya taifa," alisisitiza.

Kuhusu mchango kutoka kwa walipa kodi wakubwa, Mwenda alibainisha kuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa robo ya kwanza.

Kamishna wa Walipakodi Wakubwa, Michael Muhoja, alisema takribani asilimia 43 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa na TRA yalitoka kwa wafanyabiashara wakubwa.

"Ningependa kutoa shukrani zangu kwa walipakodi wakubwa wote kwa ushirikiano wao. 
“Tumefanya kazi kwa karibu kutoka Julai hadi Septemba, na kujitolea kwao kufuata sheria kumekuwa muhimu kwa mafanikio yetu," alisema Muhoja.