Mfumo ukusanyaji taka kidigitali waja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:31 AM Oct 19 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis
Picha: Mtandao
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis

OFISI ya Makamu wa Rais iko katika mpango wa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa taarifa za taka ngumu na taka hatarishi katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Mfumo huo utasaidia kukusanya taarifa kwa ufanisi, kuchakata maombi ya vibali na kutoa taswira halisi itakayosaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusiana na usimamizi wa taka zinazozalishwa.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, alisema hayo jana alipowasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa mfumo huo wakati wa kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma.

Alisema mfumo huu utasaidia kubaini sifa, uwezo na vifaa vya kukusanyia na kusafirisha taka vinavyotumiwa na kampuni zilizopewa kandarasi na halmashauri katika usimamizi wa taka ngumu katika maeneo yao.

Khamis alibainisha kuwa kupitia mfumo huu, serikali itapata taarifa sahihi za hali ya mazingira, changamoto zilizoko na jitihada zake kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha mfumo wa usimamizi taka nchini na hivyo kulinda mazingira na afya ya jamii.

“Mfumo huu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za usimamizi wa taka ngumu na taka hatarishi nchini. Ni matarajio yetu kuwa, mfumo utasaidia kukuza ufanisi, ufuatiliaji, uwajibikaji na kuimarisha jitihada za uhifadhi, utunzaji na usimamizi wa mazingira,” alisema.

Aliongeza kuwa mfumo huo unaoandaliwa chini ya mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Maandalizi yake yamefikia 60 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka ujao wa fedha.

 Naibu Waziri alitaja hatua zinazofuata ni kuendelea kushirikisha wadau ili kubaini mahitaji mengine yanayohitajika kwenye mfumo ikiwamo Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kuukamilisha na kuuboresha kutokana na maendeleo ya teknolojia.

Mfumo utashirikisha watumiaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), halmashauri, makandarasi na wadau wengine wanaohusika na usimamizi, ukusanyaji na usafirishaji wa taka zinazozalishwa.

Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wake, Mhandisi Stella Manyanya, imeonesha kuridhishwa na uanzishwaji wa mfumo huo.

 Mhandisi Manyanya pamoja na wajumbe wengine akiwamo Prof. Sukurani Manya, walisema kuna umuhimu wa kutoa na elimu na kuhamasisha wananchi kutenganisha taka ngumu.