RIPOTI MAALUM: Utapeli viwanja, mashamba ulivyoacha maumivu

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:58 AM Oct 19 2024
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.
Picha: Mtandao
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.

WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali nchini wamedai kutapeliwa na dhulumiwa viwanja na mashamba yao na kampuni inayojihusisha na biashara hiyo ijulikanayo kama Mzalendo Properties yenye ofisi zake Dar es Salaam.

 Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Suzan Kilamile, akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni, anasema mwaka 2021 alisikia katika chombo kimoja cha habari cha dini (jina limehifadhiwa) tangazo la kampuni hiyo la uuzaji mashamba yaliyoko kijiji cha Buyuni, Vigwaza mkoani Pwani, ndipo akashawishika kuitafuta ili kupata utaratibu.


Anasema aliwasiliana na Ofisa Masoko wa kampuni hiyo aliyemfahamu kwa jina moja la Judy, ambaye alimwelekeza kufika katika ofisi zao zilizoko katika jengo la Millenium Tower, Makumbusho, Dar es Salaam, kwa ajili ya maelezo zaidi.


Kilamile anasema alikwenda katika ofisi hizo na kuelezwa utaratibu  ikiwamo kupelekwa katika maeneo ili kuchagua kiwanja au shamba analotaka na kisha kukabidhiwa baada ya kumaliza malipo yote ya Sh. milioni moja.


Anasimulia kuwa Julai, 2021 akiwa na wenzake watano, walipelekwa Buyuni kwa ajili ya kukagua maeneo na baada ya kuridhika alichagua mashamba mawili, moja la kwake na lingine la mdogo wake.


“Sikuwa na wasiwasi wowote kwa sababu baada ya muda tulikwenda tena katika mashamba hayo na kukuta yamepimwa na wakatuonesha ramani,” anasema.


Kilamile anasema baada ya kuridhika, mwezi huo alianza malipo ya Sh. 100,000 ya kila mwezi na kumaliza Julai, 2022 kisha akampigia simu ofisa masoko huyo kwa ajili ya kumkabidhi shamba kama mkataba unavyoeleza.


Anasema baada ya hapo usumbufu ulianza na alipowapigia wahusika akiwamo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, David Mzalendo, alipewa ahadi za kukabidhiwa eneo lake lakini hakuna kilichofanyika. 


“Baada ya kuwatafuta kwa njia ya simu miezi mitatu bila mafanikio, nilikwenda katika ofisi zao zilizoko Makumbusho, nikakuta zimefungwa. Mlinzi wa eneo lile aliniambia kuwa walishahama katika jengo hilo na hafahamu waliko,” anasema.


Baada ya ahadi za takribani miezi mitatu, anasema alikwenda katika Ofisi ya Kijiji cha Buyuni kujua ukweli wa mambo ndipo Mwenyekiti wa Kijiji hicho, alipomweleza kuwa eneo analozungumzia ni mali ya mtu mwingine.


Anasema mwenyekiti huyo alipomtaka atoe nyaraka ya shamba aliyopewa na kampuni hiyo ili azifanyie kazi, hakuna majibu yoyote hadi sasa.


Mama huyo mwenye wajukuu alioachiwa na mtoto wake aliyefariki dunia miaka sita iliyopita, anasema kinachomuumiza ni kwamba alinunua shamba hilo kwa ajili ya wajukuu zake.


Oktoba 7, mwaka huu, Nipashe ilipomtafuta Mzalendo kwa njia ya simu, alidai kuwa shamba la mama huyo lipo, tatizo ni muda wa kumpeleka eneo husika hajapata.


Hata hivyo, mkurugenzi huyo alimwomba mwandishi amweleze mama huyo kuwa ampigie simu jioni ili kumsaidia kwa sababu muda huo hana nafasi ya kuzungumza naye.


“Tatizo (la) hao wateja huwa tunawaambia kila siku ukipelekwa katika eneo lako siku ya kwanza shika ramani, maeneo yao yapo ila muda wa kuwapeleka ndio unakosekana, mwambie anitafute jioni nitazungumza naye,” anasema.


Ilipofika saa 12: 42 jioni, Kilamile anasema alipompigia simu mkurugenzi huyo, alidai kwamba yuko barabarani, hivyo akitulia atamrudia lakini hakufanya hivyo hadi kesho yake alipomtafuta tena na kujibiwa kuwa, ‘nipo msibani, nitakupigia nikitulia.’


Kilamile anasema tangu siku hiyo anapopiga simu hiyo haipokewi, lakini akipiga kwa namba tofauti anapokea na kutoa majibu, hayupo sehemu nzuri atapiga akitulia.


Mkazi wa Mbeya aliyejitambulisha kwa jina Rachel, mwenye mkasa unaofanana na huo, anadai ametapeliwa na kampuni hiyo Sh. milioni 4.3 baada ya kulipia maeneo mawili tofauti yaliyogharimu Sh. milioni 1.7 na Sh. milioni 2.5.


Anasimulia kuwa mwaka 2022 alipelekwa na kampuni hiyo kuona shamba katika Kijiji cha Buyuni na aliporidhika alichukua eneo dogo lenye thamani ya Sh. milioni 1.7 na kulipa deni lote ndani ya miezi sita. alipomaliza alipewa mkataba unaoonesha kuwa amekamilisha malipo, hivyo anastahili kukabidhiwa eneo.


“Nilipokabidhiwa mkataba nikajenga imani na kampuni hii, niongeze eneo lingine lenye thamani ya Sh. milioni 2.2, Ofisa Masoko wa Kampuni hii akanihakikishia kuwa nitapata eneo pembeni ya lile la mwanzo, nililipa fedha zote kwa mara moja,” anasimulia.


Anasema akijiandaa kukabidhiwa eneo lake, alipigiwa simu na mwenzake waliyekuwa pamoja siku walipopelekwa kuoneshwa viwanja na kumweleza kuwa inaonekana kuna changamoto katika eneo hilo.


Rachel anasema alipomrejea ofisa masoko kumweleza alichosikia, alimtaka apuuze habari hizo si za kweli.


“Nilifunga safari mpaka katika kiwanja ndipo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji akaniambia eneo hili ni mali ya mtu mwingine na sisi hatutambui,” anasema.


Anasema  baada ya taarifa hizo alipomtafuta tena ofisa masoko wa kampuni hiyo, alikiri kuwapo kwa  tatizo hilo na kwamba, wanalishughulikia na baada ya hapo kila akiwatafuta wamekuwa wakimsumbua bila mafanikio.


Joyce Nkya, mkazi wa Sumbawanga, anadai kuwa ametapeliwa Sh. milioni moja kwa utaratibu unaofanana na wenzake, baada ya kulipia eneo alilooneshwa na kampuni hiyo mwaka 2022 wakati huo akiishi Dar es Salaam.


“Niliambiwa kampuni imesajiliwa serikalini. Tangu nianze kudai fedha zangu ni mwaka sasa ninazungushwa, nikipiga simu haipokewi, nikipiga kwa namba nyingine inapokewa na kuzunguzwa.


MWENYEKITI ASIMULIA
Mwenyekiti wa Kijiji cha Vigwaza, Ramadhani Kirumbi, alipotafutwa alisema alipokea wageni katika ofisi yake wakimtaka akawaoneshe maeneo yao waliouziwa na kampuni hiyo, jambo ambalo lilimshangaza kwa kuwa hakuwa na taarifa yoyote.


Alisema alipofuatilia suala hilo aligundua kampuni hiyo iliingia mkataba wa kisheria mahakamani wa kununua eneo lenye ukubwa wa ekari 11 kwa Sh. milioni 80 kutoka kwa mkazi wa kijiji hicho, Amina Mukinda.


Kirumbi alisema kampuni hiyo ililipa Sh. milioni 15 ndani ya muda waliokubaliana na ndipo Amina aliporudi mahakamani na mahakama ikaamua mkataba huo uvunjwe na eneo kurudishiwa kwa mmiliki na hivyo, kampuni hiyo ilipewa eneo lenye ekari mbili kufidia fedha waliokwisha lipa.


Alisema baada ya kugundua ukweli huo, aliwasaidia waliotapeliwa kumtafuta na kumkamata mkurugenzi wa kampuni hiyo na alipokamatwa alithibitisha kuwa alitaka kununua eneo hilo, lakini alishindwa kutimiza makubaliano hivyo si mmiliki wa ardhi hiyo.


“Baada ya kumbana, Mzalendo alitoa lile eneo la hekari mbili na kuwagawia wale waliokuwapo siku aliyokamatwa na eneo lote likaisha. Ninashangaa idadi ya watu wanaokuja kudai maeneo yao bado inaongezeka wakati hakuna lililobaki,” alisema.


Alisema kuwa anashindwa kuwasaidia watu hao kwa sababu ofisi yake haina taarifa za mauziano hayo na kuwashauri wanapokwenda kuuziwa maeneo vijijini wahakikishe wanakabidhiwa kwenye ofisi za vijiji ili wajue ukweli wa ardhi inayouzwa.


“Kama watu hawa wangepita katika ofisi yangu wasingefikia hatua ya kutapeliwa, lakini wamepeana juu kwa juu, changamoto hiyo ipo sana, kuna viwanja vinatangazwa kwenye maspika huko kuwa kuna viwanja  vinauzwa, lakini sisi wa huku vijijini tunajua wala haviuzwi,” alisema.