Anayedaiwa kumuua mke afariki akipatiwa matibabu

By Moses Ng’wat , Nipashe
Published at 12:22 PM Oct 19 2024
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi (ACP) Johnny Maro
Picha: Mtandao
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi (ACP) Johnny Maro

ALLY Mwakilembe (45) anayedaiwa kumuua mke wake, Wema Ndile (32) ambaye walitengana kwa miezi mitano kwa kumchoma visu, amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu.

Mwakilembe anadaiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, naye alijichoma kisu tumboni kisha kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, kwa matibabu na alifariki dunia juzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi (ACP) Johnny Maro, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alisema wawili hao ni wakazi wa kijiji cha Kapeta, Kata ya Ikinga, Ileje mkoani Songwe.

Alisema tukio la mauaji hayo lilitokea Jumanne usiku katika kijiji cha Kapeta ambapo Mwakilembe alimshambulia kwa kumchoma visu Ndile sehemu za shingoni na ubavuni upande wa kulia akiwa nyumbani kwake na kusababisha kifo.

“Baada ya tukio hilo, Mwakilembe naye alijichoma kisu tumboni na kujisababishia jeraha. Alipelekwa  Hospitali ya Wilaya ya Ileje na siku mbili mbele, majira ya saa 9:30 alfajiri, alifariki dunia,” alisema.

Alisema wawili hao walikuwa mke na mume ambao walitengana miezi mitano iliyopita na mke alikwenda kuishi sehemu nyingine.

Kamanda Maro alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Maro alitoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepusha kutokea kwa matukio mabaya kama ya mauaji.

Taarifa iliyotolewa awali na Mtendaji wa Kijiji cha Kapeta, Octatus  Wangu, ilisema kabla ya mauaji hayo kutokea, mtuhumiwa alikuwa katika harakati za kumshawishi mtalaka wake amrudie baada ya kutengana kwa miezi mitano.

Alisema ndoa ya wawili hao ilidumu kwa kipindi cha miaka 10 na kupata watoto wawili lakini baadaye mwanamke aliamua kutengana na mumewe akimtuhumu kuzidisha ulevi na kusahau majukumu ya familia.