Mageuzi bandari kuifanya Zanzibar kitovu muhimu upokeaji mizigo ya nje

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:10 AM Oct 19 2024
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mapinduzi makubwa katika miundombinu ya bandari yanalenga kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha usafirishaji na kupokea meli kubwa zinazoingiza bidhaa nchini.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano, Ikulu, Zanzibar, ilisema Rais Mwinyi alisema hayo jana alipoifungua bandari kavu ya Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema ufunguzi wa bandari kavu ni hatua muhimu ya kuimarisha utendaji wa bandari kwa kuwa itapunguza msongamano wa shehena yakiwamo makontena katika Bandari ya Malindi.

Rais Dk. Mwinyi, kwa mujibu wa taarifa hiyo, alisema mabadiliko hayo ya miundombinu ya bandari yataleta msukumo mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na kuwasisitiza wadau kuunga mkono juhudi hizo.

Alisema kampuni ya Africa Global Logistic inayoendesha bandari ya Malindi hivi sasa inaendelea kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji yanayoongeza ufanisi na kuwapa urahisi wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao bila usumbufu na kuokoa muda.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia wadau kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)  itaendelea kufanya kazi zaidi na sekta binafsi kwa kuwa mbali ya kuwa na mitaji, pia inakuja na utaalamu na teknolojia za kisiasa zinazochochea ufanisi kwenye utendaji.

Taarifa hiyo ilisema Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kwa kuifanya kuwa yenye uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi zikiwamo kampuni za kimataifa kuleta meli za mafuta kwenye bandari hiyo.

Alisisitiza kuwa  bado kuna fursa zaidi za kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa bandari zote na kuziagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), Taasisi ya Nguvu za Atomiki na Mkemia Mkuu wa Serikali kuongeza kasi na ufanisi katika utendaji ili kuwarahisishia wafanyabiashara mazingira bora ya ufanyaji wa biashara yatakayopunguza gharama na kumpa unafuu mtumiaji.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, imedhamiria kuendesha huduma za bandari kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia bandari ni lango kuu la uchumi kwa nchi.
Pia alisema serikali kupitia mradi huo utawapunguzia gharama kubwa wafanyabiashara.

Alisema hatua hiyo pia itasaidia harakati za uendeshaji kuwa zenye ufanisi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uletaji mizigo (freight price) ndani ya nchi.

Rais Dk. Mwinyi pia aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali  inaendelea kuwawekea mazingira rafiki hasa kwa ujenzi wa miundombinu. 

Alisema serikali inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuendeleza sekta ya uchukuzi na kuimarisha jitihada za pamoja za kuleta mafanikio ya kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege Unguja na Pemba ili kuwarahisishia huduma wananchi na wageni wanaoitembelea Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliwasihi wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa kuwazingatia wananchi hasa kuwapunguzia makali ya bei za bidhaa kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali za kupunguza gharama za usafiri.

Waziri wa Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhammed amesema, mageuzi na mafanikio yaliyofikiwa kuimarisha bandari ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025.

Alisisitiza kuwa mabadiliko yanayoendelea kwa kuziimarisha bandari, yataifanya Zanzibar kufikia malengo na matarajio ya kuhudumia meli takriban laki tatu kwa mwaka.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Atif Khamis, alisema  dhana ya ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi imechochea mabadiliko makubwa ya utendaji wa bandari.

Alisema ufunguzi wa bandari kavu utaongeza mapato ya shirika na kupunguza msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi.
Atif alisema kumekuwa na ongezeko la mapato kwa asilimia 15 tangu kampuni binafsi kuingia ushirikiano na serikali kuiendesha Bandari ya Malindi, kupungua kwa muda wa meli kusubiri gati kwa asilimia 75 na muda wa kutoa makontena kutoka siku 40 hadi siku saba hadi 10 hivi sasa kwa asilimia 50.