Wawili hufariki kila mwezi Ziwa Victoria

By Rose Jacob , Nipashe
Published at 02:21 PM Oct 19 2024
Ziwa Victoria.
Picha: Mtandao
Ziwa Victoria.

TAKRIBAN wawili hufariki dunia kila mwezi Bunda mkoani Mara, kutokana na ajali mbalimbali za majini wakati wananchi wakifanya safari na shughuli za kiuchumi ndani ya Ziwa Victoria.

Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Vicent Naano, wakati akipokea msaada wa vifaa okozi hususani jaketi 20 kutoka Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kutokana na ajali ya mtumbwi iliyotokea Septemba 15 katika Kijiji cha Igundu na kusababisha vifo vya watu sita. 


Dk. Naano alisema asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo, uchumi wao unategemea Ziwa Victoria na suala la usafiri au shughuli zao ndani ya ziwa ni jambo la kawaida ambalo linakabiliwa na adha ya ajali za mara kwa mara zinazosababisha vifo wilayani humo.


"Tunapokea watu wengi. Kila  mwezi lazima kunatokea vifo na tayari tumebaini kuwa vifo vingine vinatokana na watu kutozingatia  sheria za usafiri salama majini.  Tumeanza  kampeni maalum ya kuelimisha jamii kuzingatia suala zima la usalama wawapo majini," alisema Dk. Naano.


Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Masinde Bwire, alisema ofisi yake imetoa msaada wa vifaa okozi kutokana na ajali iliyotajwa ya mtumbwi uliokuwa umebeba abiria wakitokea harusini na watu sita kufa maji na wengine 14 kunusurika baada ya mtumbwi huo kuzidiwa na mzigo huku ikidaiwa kuwa haukuwa maalum kwa kusafirisha abiria.


Alisema kuna haja ya mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ajali ambazo zimeendelea kutokea ndani ya ziwa hilo na kusababisha vifo vya watu wengi kila mwaka nchini pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.


Bwire alisema kamisheni hiyo tayari imeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya uokozi katika nchi zote tatu, huku kituo kikuu kikijengwa mkoani Mwanza na vitakapokamilika pamoja na mambo mengine vitasaidia kupatikana taarifa kwa haraka za ajali na uokoaji kufanyika mapema.


Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Igundu, wilayani humo, akiwamo Nyanjiga Mafuru, walisema ili kukomesha ajali hizo hatua kali zichukuliwe dhidi ya wamiliki wa mitumbwi ya uvuvi wanaoitumia kusafirisha abiria wakijua leseni zao sio za usafirishaji bali ni za uvuvi.