Majaliwa ataja umuhimu wa NIDA katika matumizi ya mifumo kidigiti

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 02:48 PM Oct 19 2024
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mtandao
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kila Mtanzania ambaye hajapata namba za NIDA ajiandikishe kwa sababu ni muhimu kuwa nayo wakati huu wanapotumia mifumo ya kidijitali ambayo inasomana na NIDA.

Majaliwa aliyasema hayo juzi wakati akifunga Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo la siku tano ambalo lilihusisha wadau wa TEHAMA wa ndani na nje ya nchi, limeandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya TEHAMA.

Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan alisema, “Kama utafiti unavyoonesha, hadi mwaka 2030, shughuli nyingi zinazofanywa kwa mkono zitaboreshwa na kuwa za kidijitali.”

Alisema matumizi ya teknolojia hizo yanaweza kuathiri uaminifu pamoja na masuala ya kimaadili yanayozunguka faragha, umiliki na uwazi.  

Kwa  muktadha huo, alisema serikali na wadau wote hawana budi kuweka mikakati ambayo itaweza kudurufu matumizi chanya ya teknolojia hizo ambazo kutokana na umuhimu wake haziwezi kukwepeka.

Majaliwa aliitaka wizara husika pamoja na wadau wote kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Nchi yanayohusu kuunganisha mifumo yote ya TEHAMA.

Pia aliiagiza wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati kutekeleza kwa wakati ujenzi wa Chuo cha TEHAMA mkoani Kigoma.

“Wizara isimamie na kuhakikisha ujenzi wa Vituo vya Ubunifu (Innovation Hub) katika mikoa iliyokubalika unafanyika kama ilivyopangwa,” aliagiza.

Pia aliitaka Tume ya TEHAMA ikamilishe mchakato wa kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT Refurbishment and Assembly Centre).

Kadhalika aliitaka tume hiyo kuendelea kuboresha mfumo wa kuwatambua na kuwasajili wataalamu wa TEHAMA nchini.

Alisema serikali katika mwaka 2020 ilizindua mfumo wa N-Card ambao hadi kufikia sasa imefanikiwa kuwaunganisha wananchi wasiopungua milioni nne.

“Mfumo huu umesaidia sana kuokoa upotevu wa fedha katika vivuko vya Magogoni na Kivukoni. 
“Vilevile, mfumo huo umesaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwenye Kituo cha mabasi cha Magufuli na katika viwanja vyetu vya mpira,” alisema.

Alisema serikali inaendelea kutekeleza wa Mpango mkakati wa miaka mitano 2024/25 – 2029/30 wa anga za juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, alisema serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambapo kwa mwaka fedha 2023/24, jumla ya urefu wa kilomita 1,592 za mkongo wa taifa zimejengwa na kufika katika wilaya 83.

Pia alisema umoja wa watoa huduma za mawasiliano wamejenga jumla ya kilomita 2,595 ambazo zinafanya mkongo wa taifa kuwa na kilomita 13,820.

Silaa alisema wizara imehamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano na Kituo cha Kuhifadhia Data (NIDC) kwenda katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk. Nkundwe Mwasaga, alisema: “Siku ya pili ya kongamano walikuja vijana wa sekondari wa shule za mchepuo wa Kiingereza na Kiswahili wakaonesha uwezo mkubwa katika teknolojia ya roboti. Imewavutia watu wengi wa ndani na nje ya nchi.” 

Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD), Nardos Bekele-Thomas, alimpongeza Rais Samia kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha Tanzania inatumia ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika kuchagiza Maendeleo Endelevu nchini.

Katika kongamano hilo Watanzania ni miongoni mwa waliopewa tuzo kupitia mashindano ya vijana wa Afrika walionesha ubunifu zao katika matumizi ya akili mnemba na roboti.

Majaliwa aliwataka wataalamu wa TEHAMA kujadili namna teknolojia hizo zitakavyotumika kufikia mapinduzi ya nne, tano na sita ya viwanda na hatimaye kuondoa mitazamo kinzani iliyoko kwenye jamii.