TARI yatoa mafunzo kwa wakulima, maofisa ugani

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:15 AM Sep 21 2024
Mkulima
Picha: Mtandao
Mkulima

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele imeanza kutoa mafunzo kwa wakulima na maofisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida kuhusu kilimo cha korosho ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo litakalowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo yalianza kutolewa juzi katika shamba la mkulima Mustapha Mwangi lililoko Kata ya Ilongero, lengo likiwa kupunguza athari za wadudu na magonjwa yanayoweza kupunguza uzalishaji na tija ya zao hilo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mtafiti kutoka TARI, Gaspar Mgimiloko alisema wameanza kutoa mafunzo hayo kwa wakulima ili kutambua umuhimu wa matumizi sahihi na salama ya viwatilifu ili kudhibiti visumbufu vya korosho.

Alisema wakulima hao watafundishwa namna ya upuliziaji viwatilifu, matumizi ya mavazi kinga, mbegu bora, utunzaji shamba, uchanganyaji mazao na upogoleaji.

Mgimiloko alisema mafunzo haya ni muhimu kwa maofisa hao hasa wale waajiriwa wapya, ili kuongeza uelewa wao kuhusu uzalishaji korosho, hususan wanaotoka maeneo ambayo hayana uzoefu na zao hili.

"Lengo la kuwajumuisha wakulima na maofisa ugani, tunaamini maofisa ugani tayari wana mafunzo walioyapata vyuoni, lakini kuna maofisa ugani ambao ni waajiriwa wapya yamkini wanatoka sehemu au kanda ambazo hazilimi korosho, lengo pia ni kuwaongezea wigo wa uelewa juu ya uzalishaji zao la korosho," alisema.

Mkulima Emiliana Lisu kutoka Kata ya Kinyagigi, aliahidi kuyafanyia kazi mafunzo aliyoyapata ikiwa ni pamoja aina na matumizi sahihi ya viuatilifu, namna nzuri ya upandaji korosho pamoja na ujuzi kuhusu udongo unaofaa.

Mmiliki wa shamba lililotumika kwa mafunzo, Mwangi, alieleza namna mafunzo yalivyomsaidia kufahamu thamani ya kilimo cha korosho na kuboresha shamba lake ambalo awali halikutoa mavuno mazuri.