Pindi azindua utalii wa puto Hifadhi ya Ruaha

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 01:02 PM Oct 08 2024
   Pindi azindua utalii wa puto Hifadhi ya Ruaha
Picha:MPigapicha Wetu
Pindi azindua utalii wa puto Hifadhi ya Ruaha

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi, Dk. Pindi Chana, amehitimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kuzindua utalii wa puto.

Uzinduzi huo umefanyika jana katika eneo la Korongo View ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha, mkoani Iringa.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Dk. Chana alisema mafanikio hayo ni kutokana na jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii.

"Tunamshukuru Rais Samia kwa kuionesha dunia vivutio vya utalii vya Tanzania ambapo mpaka sasa watalii wameongezeka na kufikia milioni 1.8 na mapato ya Taifa tunachangia asilimia 17 na fedha za kigeni takribani Dola za Kimarekani bilioni 3.6.

Kuhusu maboresho ya miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, Dk. Chana alisema kuwa hadi sasa kuna barabara ya Iringa-Msembe yenye urefu wa kilomita 104 ambayo inaenda kujengwa.

Alisema katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kutakuwa na uwanja wa ndege sambamba na kutumia uwanja wa ndege wa Nduli ulioko Mkoa wa Iringa ambao unaendelea kukarabatiwa.

Aidha, alisema kwa miaka mitatu kumekuwa na mabadiliko makubwa ya sekta ya utalii na serikali inazidi kuboresha maeneo mengi ya utalii huku akihamasisha wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika hifadhi hiyo ya Ruaha.

Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii inafanya kazi kubwa kusimamia hifadhi zote 21 nchini kuona zinaendelea kuwa tegemeo kubwa kwa taifa.

Alisema wizara hiyo ipo kutekeleza 4R za Rais Dk. Samia na ndio maana hailali inapiga kazi.

Kuhusu Hifadhi ya Ruaha, alisema ni moja kati ya hifadhi kongwe nchini na mafanikio makubwa yameonekana kupitia miaka 60 ya kuanzishwa kwake.

Alisema hifadhi za taifa zinatoa mchango mkubwa kwa taifa kwenye nyanja mbalimbali na kuwa Pato la Taifa limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wahifadhi wastaafu wa hifadhi hiyo, Loriviole Moirana, waliitaka serikali kuendelea kuikumbuka hifadhi hiyo kwa kutenga fedha za uendeshaji na kuzituma kwa wakati ili ziweze kusaidia kuendesha hifadhi pia kuwe na ndege zaidi ili kusaidia kupambana na matukio ya ujangili pamoja na uendeshaji wa hifadhi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, alisema Hifadhi ya Ruaha ni muhimu ambayo imefanya mkoa kuendelea kutangazika kupitia utalii.

Alipongeza wadau mbalimbali wa utalii ikiwamo kampuni ya Foxes ambao ndio waasisi wa utalii katika hifadhi hiyo.

Alisema kupitia jitihada za wadau wa utalii, hifadhi hiyo imepiga hatua kwa kuanzisha utalii wa puto.

Pia, alisema serikali imeendelea kufanya jitihada kubwa kwa kufungua utalii kwa kupitia filamu ya The Royal Tour pamoja na mradi mkubwa wa Regrow ambao unajenga viwanja vya ndege viwili; kiwanja cha Iringa na kiwanja cha Msembe pamoja na ujenzi wa lami kilomita 104.