Mpina amtwisha Nchimbi kero za wafugaji, wakulima

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 12:54 PM Oct 08 2024
Mpina amtwisha Nchimbi kero za wafugaji, wakulima
Picha: Mpigapicha Wetu
Mpina amtwisha Nchimbi kero za wafugaji, wakulima

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, jana ameibua kero tatu za wakulima na wafugaji, akimtaka Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi kuitaka serikali kuzitatua ili wananchi wapate haki yao.

Kero hizo ni wafugaji waliokamatiwa mifugo yao kushinda kesi, lakini hadi sasa haijarejeshwa, wakulima kutozwa Sh. 300 katika kilo moja ya pamba kwa ajili ya kugharamia pembejeo na kilo moja ya mbegu kuuzwa Sh. 10,000 hali inayowakosesha haki wakulima.

Alisema wafugaji ambao mifugo yao ilitaifishwa na kushinda kesi mahakamani miaka mitatu iliyopita, mpaka leo hawajalipwa.

Mpina aliyasema hayo jana mjini Meatu mkoani Simiyu.

Akijibu hoja hizo, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hatovumilia jambo lolote litakalofanywa kinyume cha sheria na viongozi wa serikali kwa kuwa yeye ni muumini wa utawala wa sheria.

"Nitalibeba suala hilo mpaka nihakikishe haki yao imepatikana kama walishinda kesi mahakamani hatupaswi kuwakimbia," aliahidi Nchimbi.  

Mpina pia, alilalamikia kuwapo kwa wakulima wa pamba wanaokatwa Sh. 300 kwa ajili ya viwatilifu na kuuziwa mbegu ya mahindi kwa Sh. 10,000 kwa kilo.

Kutokana na hoja hiyo, Nchimbi alimtaka Mkuu wa Mkoa Simiyu, Kenani Kihongosi kujibu hoja hiyo na kusema: "Serikali inakwenda kutoa ruzuku mbegu za mahindi na watapata mbegu kwa bei nafuu.”

“Suala la pamba nimelibeba na wataenda kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo na kwamba serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba wanaendelea kuangalia namna ya kumaliza tatizo hilo," alisema Kihongosi.

Aliwatuhumu baadhi ya wanasiasa kupewa mbegu kuzigawa kwa wakulima, lakini walikuwa wanampa kila mwananchi na asiye mkulima jambo lililochangia wengi kukosa.

"Hawa wanasiasa tumepiga marufuku endapo tutabaini hilo tena awe ni diwani au mwenyekiti tutachukua hatua za kisheria," alisema.

Hata hivyo, Mpina hakuridhika na majibu hayo na kunyoosha mkono, na alipopewa nafasi na Nchimbi alisema alichokisema mkuu huyo wa mkoa kuhusu wanasiasa kugawa mbegu sio kweli na kwamba hakuna viongozi wa siasa waliofanya hivyo.

Aidha, alisema msimamo wake anataka kujua kwanini mbegu ya mahindi iuzwe kilo moja kwa Sh.10,000 na kipi kisababishi cha kufikia bei hiyo.

“Kuwasingizia wanasiasa ni kuwasingizia tu hakuna mwanasiasa anayegawa mbegu, aseme ni mwanasiasa gani ambaye huwa anasimama kugawa mbegu maana hili la mwanasiasa limekuwa kama haramu," alisema Mpina huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wamefurika eneo hilo.

Nchimbi akijibu, alisema chama chake kitaendelea kutetea wananchi wanyonge na kuwashirikisha katika masuala yote muhimu.

Aidha, alisema wananchi na viongozi wengine wanapaswa kumzoea Mpina akikumbushia alikuwa mbishi tangu wakiwa chuo wanasoma.

Akiwa Bariadi juzi, Nchimbi alisisitiza umoja, amani na mshikamano na kwamba hiyo ndio njia ya kuliunganisha taifa.

“Watanzania wa vyama vyote tunapaswa tujue jambo ambalo tulilonalo lenye thamani kubwa ni amani, umoja, mshikamano wa taifa letu," alisema Nchimbi. 

Aidha, alisema kila anayejaribu kuuvuruga umoja aambiwe kwa macho makavu kwamba hatupo tayari kuvumilia nchi iingie katika machafuko.

Akizungumzia miradi mikubwa ya maendeleo iliyofanikiwa ikiwamo Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, alisema hakuna mtu aliyeamini kwamba baada ya kuondoa Rais Dk. John Magufuli hakuna mtu atakayeweza kuumaliza.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo kuwa anapenda watu wake kwa kuhangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo na kusimamia kuhakikisha inatekelezwa.

“Kwa hiyo kazi tuliyonayo ni ya kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kuitumikia nchi yetu kwa uaminifu, upendo mkubwa na nchi yetu iendelee kupata maendeleo,” alisema Nchimbi. 

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, alisema chama hicho kitatumia mfumo wa KKK (Kuhamasisha, Kujiandikisha na Kuweka Mawakala).

Aidha, alitoa wito kwa wananchi ifikapo Oktoba 11 hadi 20, mwaka huu, wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la mkazi ili waweze kushiriki katika uchaguzi huo na kwamba chama kitaleta wagombea wenye sifa.