Mavunde awataka wananchi kutunza miradi ya maendeleo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:53 PM Oct 08 2024
Mavunde awataka wananchi kutunza miradi ya maendeleo
Picha:Mpigapicha Wetu
Mavunde awataka wananchi kutunza miradi ya maendeleo

WAZIRI wa Madini, Antony Mavunde amewataka wananchi wa Wilaya ya Chato kutunza miundombinu ya maendeleo,inayojengwa ili idumu na kuwa na tija kwa vizazi vijavyo kwakuwa serikali inatumia gharama kubwa kutekeleza miradi hiyo.

Waziri Mavunde ameyasema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika barabara ya Kahumo –Bus terminal yenye urefu  wa Km moja iliyojengwa kwa kiwango cha lami katika kata ya Muungano Wilayani Chato Mkoani Geita iliyogharimu zaidi ya Sh.milioni 945.

Amesema serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya elimu,afya ,maji na miundombinu ya barabara hivyo ni vyema wananchi wakailinda na kuitunza kwakuwa ni moja ya fursa za kiuchumi katika maeneo yao.

Mbali na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara,Waziri Mavunde pia ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi  wa upanuzi wa Shule ya Sekondari Makurugusi inayojengwa madarasa ya kidato cha tano na sita ili kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika maeneo hayo kuendelea na masomo.

Amesema ujenzi wa shule hiyo inayojengwa kwa gharama ya Sh. milioni 919.4 utawaondolea adha wananchi waliokuwa wakichaguliwa kwenda kidato cha tano na sita na kushindwa kwenda kutokana na kutomudu gharama za usafiri kwakuwa shule ziko mbali na maeneo hayo.

“Serikali inatoa elimu bure lakini ili mwanafunzi aweze kusoma lazima asafiri kwakuwa maeneo haya hayana shule ya kidato cha tano na sita, lakini ujenzi huu unakuwa mwarobaini wa changamoto hii na sasa wanafunzi watamaliza kidato cha nne na wataweza kuendelea na kidato cha tano bila usumbufu,”amesema Mavunde.

Amesema dhamira ya serikali ni kuona wanafunzi wanasoma kwenye mazingira rafiki na wezeshi na kwamba elimu bure imeondoa kero ya wazazi kulipa kulipa ada waliyokuwa wanakabiliana nayo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema kwa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Serikali imejenga shule 180 kwa shule za msingi na sekondari ambazo zimesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu.

Katika kipindi hichohicho Serikali imetoa zaidi ya Sh. bilioni 800 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kwa Wilaya ya Chato pekee zaidi ya Shilingi bilioni 109  zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu,afya,maji na miundombinu ya barabara.

Diwani wa Kata ya Muungano,  Kapembe Charles  akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, lakini bado wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara uliosababishwa na mvua za masika.

Mbali na ubovu wa barabara amesema katika eneo hilo wananchi wanakabiliw ana changamoto kubwa ya maji,hali inayowalazimu wannachi kutumia maji ya visima vya kuchimba kwa mkono ambayo sio salama kwa afya zao.

Diwani Charles amesema kutokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya wananchi wa kata hiyo walilazimika kujenga maboma ya zahanati kwenye vijiji vitano vya kata hiyo na wameyakamilisha hadi lenta, lakini wameshindwa kukamilisha na kuimba Serikali kukamilisha ujenzi huo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya karibu.

Baadhi ya wananchi Musa Petro na Renatha Samuel kwa nyakati tofauti wamesema kukamilika kwa barabara hiyo kumewarahisishia gharama za usafiri kwa kuwa awali walilazimika kupanda pikipiki kwa Sh. 5,000 lakini sasa imeshuka hadi kufikia Sh. 2000.