MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya tuhuma ya kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inayomkabili wanandoa Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54), baada ya washtakiwa hao kuongeza wakili mwingine wa kuwatetea.
Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.
Wakili wa Serikali Faraja Ngukah alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na pia wanashahidi mmoja wapo tayari kuendelea.
Baada ya Ngukah kudai hayo, Wakili Mnyele aliieleza Mahakama kuwa washtakiwa wameongeza wakili ambae ni yeye, kwa hiyo anaomba apewe muda ili aweze kupitia mwenendo wa kesi tangu imeanza hadi ilipofikia.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilikubaliana na ombi la Wakili Gabriel Mnyele , ambapo pande zote zilikubalina kesi hiyo iendelee kusikilizwa siku mbili mfululizo Novemba 6 na 7, mwaka huu, lakini Wakili mwingine wa washtakiwa hao, Edward Chuwa alidai kuwa iwe tarehe sita, tarehe sana ana kesi Mahakama Kuu.
Wakili Ngukah aliiomba Mahakama hiyo imuonye shahidi watano katika kesi hiyo ili afike tarehe ya kesi kutoa ushahidi wake. Hata hivyo, shahidi huyo alidai kuwa na yeye ataomba udhuru kwa sababu ni mara ya tatu anafika mahakamani hatoi ushahidi amechoka.
Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hadi Novemba 6, mwaka huu kwa kuendelea kusikilizwa kwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Ilidaiwa kuwa Nathwan anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED