Mwinyi aziagiza taasisi kushughulikia kero za wazee

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:18 PM Oct 08 2024
Mwinyi aziagiza taasisi kushughulikia kero za wazee
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwinyi aziagiza taasisi kushughulikia kero za wazee

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameziagiza taasisi zote zinazotoa huduma za ustawi kwa wazee, kuzishughulika haraka na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wazee hao.

Dk. Mwinyi alitoa agizo hilo Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini, Pemba kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani.

Taasisi zilizopewa agizo hilo ni Wizara ya Afya ambayo imeagizwa kuandaa madirisha maalumu hospitali zote ya kutoa huduma za wazee kwa kuwapa kipaumbele, pamoja na kuongeza madaktari bingwa wa magonjwa ya wazee.

Pia, ameiagiza Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano kuishughulikia Sheria vya Vyombo vya Barabarani na kuharakisha mchakato wa kuwapatia wazee vitambulisho maalumu vitakavyowasaidia kulipa nusu nauli kama ilivyo kwa wanafunzi na watu wenye ulemavu.

Wizara ya Fedha imeagizwa kuandaa bajeti maalumu ya kuendesha mabaraza ya wazee pamoja na kufungua madirisha maalumu kwenye benki na huduma za fedha yatakayotoa msaada na kipaumbele kwa kuwahudumia wazee hao.

Rais Dk. Mwinyi, pia ameitaka Wizara ya Wanawake, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana taasisi na jumuiya zinazoshughulika na masuala ya wazee nchini kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuepukana na mitazamo potofu kwa kuwapachika wazee tuhuma za uchawi.

Amesema, serikali imeandaa na inaendelea kutekeleza Sera ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2014 ambayo imeweka mikakati madhubuti ya kusimamia maendeleo ya wazee.

Kadhalika, serikali imetunga Sheria ya Masuala ya Wazee namba 2 ya mwaka 2020 kwa maadhimisho ya kusimamia haki na maslahi ya wazee nchini.

Pia, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Jumuiya na Mabaraza ya Wazee katika  ngazi za Mkoa, Wilaya na Shehia inafanya kila juhudi kusimamia na kuimarisha maendeleo ya wazee nchini.

Alisema hadi sasa shehia na wilaya zote nchini zimeanzisha mabaraza ya wazee. Kwa hakika, hii ni hatua kubwa kwani mfumo huu wa kuwepo mabaraza kuanzia ngazi ya chini kabisa unasaidia katika kupeleka taarifa kwa wepesi na kurahisisha utatuzi wa changamoto pale zinapotokezea.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya Siku ya Wazee Duniani, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar itaendelea kuwapa wazee maisha yenye heshima kama wanavyotambulika kwenye Katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar.

Akisoma risala kwa niaba ya wazee wenziwe, mwakilishi wa wazee, Ali Said Mattar, ameiomba serikali kuwapa kipaumbele kwenye huduma za afya, usafiri, na benki kwa kuwaharakishia mchakato wa kuwapatia vitambulisho maalumu vitakavyowatambulisha sehemu hizo pamoja na kuwapatia nafasi maalumu za uwakilishi kwenye vyombo vya kutungia sheria ikiwamo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza wa Wawakilishi ili kuzisemea changamoto zinazowakabili.

Aidha, Wazee hao wameiomba Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Usafiri wa Vyombo vya Barabarani, Namba 7 ya mwaka 2007 kwa kuwatoza nusu nauli wazee wote kwenye usafiri wa umma kama ilivyo kwa wanafunzi na watu wenye ulemavu. Pia wamempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaongezea wazee pensheni jamii kutoka elfu 20 hadi 50 na pensheni ya wastaafu kutoka elfu 90 hadi laki moja na 80.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa "HelpAge" Smart Smart Daniel, ameisifu Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwajali, kuwathamini na kuwatunza wazee kwa kutumia gharama kubwa zaidi ya bilioni 17. 6 kwa ajili ya kulipia pensheni Jamii suala alilosema kuwa Zanzibar ni nchi ya kwanza duniani kwa Serikali kutumia gharama kubwa kwa wazee bila ya misaada kutoka nje au mashirika ya kimataifa.

Siku ya Wazee Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1991 na Tanzania hususani Zanzibar ilianza mwaka 2004 na ujumbe mahususi kila mwaka, ujumbe wa mwaka huu ni "kuzeeka kwa heshima; umuhimu wa kuimarisha matunzo na mifumo ya usaidizi kwa wazee".