Vikundi vya Kijamii Chalinze vyapigwa msasa NMB Kijiji Day Miono

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:10 PM Oct 08 2024
Vikundi vya Kijamii Chalinze vyapigwa msasa NMB Kijiji Day Miono
Picha:Mpigapicha Wetu
Vikundi vya Kijamii Chalinze vyapigwa msasa NMB Kijiji Day Miono

VIKUNDI vya Kijamii nchini vimetakiwa kuchangamkia fursa zilizomo katika Akaunti ya Kikundi ya Benki ya NMB ‘NMB Kikundi Akaunti,’ ili kuvirasmisha na kunufaika na huduma za Bima, Mikopo na Huduma Jumuishi za Kifedha Kidigitali kwa maendeleo yao kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB anayeshughulikia Mauzo ya Vikundi na Usambazaji wa Huduma za Kibenki Vijijini, Dismas Prosper, wakati wa semina ya Elimu ya Fedha kwa Watanzania waishio maeneo yasiyofikiwa na Taasisi za Kibenki inayoendeshwa na NMB.
 
Semina hiyo imeendeshwa na NMB katika Kijiji cha Miono, Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, wakati wa Tamasha la Kujenga Uelewa wa Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Watanzania, inayotolewa na Benki ya NMB 'NMB Kijiji Day,' iliyoambatana na Bonanza la Michezo mbalimbali.
 
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyoshirikisha wanachama takribani 150 wa vikundi vya kijamii, Dismas alisema NMB Kikundi Akaunti ni mwamvuli unaojumuisha huduma chanya mbalimbali zinazoweza kuharakisha ukuaji kiuchumi wa vikundi na mwanachama mmoja mmoja.
 
“Msukumo wa maboresho ya NMB Pamoja Akaunti kuwa NMB Kikundi Akaunti, ulilenga kumaliza changamoto mbalimbali zinazokwaza ustawi wa vikundi vya kijamii nchini, kutokana na uendeshwaji wa ujanja ujanja usioweza kunufaisha wanachama katika pesa za vikundi vyao.
 
“NMB Kikundi Akaunti ndio suluhisho la utunzaji fedha za kikundi, inayomuwezesha kila mwanachama kujua namna ya kunufaika na pesa zake na kumuwezesha mtu mmoja mmoja na kikundi kwa ujumla kufikia malengo na mipango katika matumizi ya pesa zao.
 
“Akaunti hii inazikusanya pamoja suluhishi mbalimbali, pamoja na kuwaelimisha wanachama namna wanavyoweza kunufaika na pesa zao kwa kununua hisa katika Masoko ya Hisa, kukopa mikopo nafuu na kukatia bima za vikundi, familia na mtu mmoja mmoja,” alisisitiza.
 

1

Dismas alibainisha ya kwamba, faida za NMB Kikundi Akaunti ni pamoja na usalama wa pesa za vikundi, ufunguzi na uwekaji akiba rahisi kidigitali, kupata taarifa sahihi na za wazi za kifedha kwa kila mwanachama na kusisitiza kuwa pesa zote mahali pake ni benki na sio kabatini au mchagoni.
 
Akaongeza ya kwamba, licha ya akaunti ya Kikundi, wanachama wa Vikundi vta Kijamii wanapaswa kujifungulia akaunti binafsi ili kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo Mshiko Fasta, mkopo usio na masharti wala ujazaji fomu unaoweza kumpatia mteja wao hadi Sh. Mil. 1.
 
Wakizungumzia mafunzo na elimu ya fedha waliyopewa katika semina hiyo, mshiriki Josephine Steven alikiri kuvutiwa na huduma ya NMB Kikundi Akaunti, na hata Bima za Vikundi, huku akiitaka NMB kuongeza kasi katika kuvifikia vikundi vya kijamii vya watu walioko vijijini.
 
“Vijijini ndiko viliko vikundi vingi vya kijamii, kupitia semina hii tumeweza kutambua namna sahihi ya kutunza pesa zetu kisasa, manufaa tunayoweza kupata kwa kurasmisha vikundi vyetu, lakini zaidi ni ile bima ya vikundi inayoweza kutoa mkono wa pole mtu anapofiwa,” alisema Josephine.
 
Naye Shaban Kwangaya, ambaye ni mjasiriamali mkazi wa Miono, alisema amevutiwa na elimu juu ya huduma za Bima ya Afya ya Vikundi waliyopewa katika semina hiyo, hasa ukizingatia changamoto kubwa kwa wakazi wa vijijini ni uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
 
“Ukiachana na Bima ya Afya, lakini pia nimejifunza mengi ambayo sikuyajua kuhusu akaunti za vikundi na mikopo ya riba nafuu, naahidi sio tu kuwa balozi mwema wa NMB kwa jamii, bali nitakuwa mtumiaji wa kila fursa inayokuja kupitia huduma za benki hii,” alisema.
 
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Kata ya Miono, Bhoke Nyitika, aliwapongeza washiriki wa semina ya NMB Kijiji Day na kwamba anaamini ikitumiwa ipasavyo na wanachama wa vikundi, elimu waliyopata itasaidia kuharakisha maendeleo ya vikundi kiuchumi na kukuza pato la kila mmoja.