‘Wafanyakazi wanatakiwa kuwa na washauri kulinda afya ya akili’

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:08 PM Oct 08 2024
Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili, kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH). Dk. Godwin Mwisomba.
Picha:Mtandao
Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili, kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH). Dk. Godwin Mwisomba.

IMESHAURIWA na wanataaluma wa afya ya akili kwamba, mahali pa kazi kuwapo ‘mentors’ (washauri), ili kuponya ‘majeraha’ ya kiakili kazini yanayowakumba wafanyakazi kama vile sonona na msongo wa mawazo.

Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili, kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH). Dk. Godwin Mwisomba, amesema takwimu za dunia zinaonesha mahali pa kazi ni eneo mojawapo la chanzo cha magonjwa ya akili.

“Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unaeleza kwenye kila wafanyakazi watano, mmoja wao ana ‘work related stress’ (msongo wa mawazo utokanao na kazi), na kusababisha magonjwa ya akili.

Pia kuna utafiti wa Deloitte wa mwaka 2022 unasema kwamba asilimia 84 ya wafanyakazi wamepitia changamoto za msongo utokanao na kazi ama mazingira ya kazi,” alisema Dk. Mwisomba.

“Utafiti wa Deloitte umegundua kwamba wazazi ambao wanajali afya ya akili ya mtoto wao walijikuta wakijitahidi kufanya vyema kazini na kuendeleza maisha yao ya nyumbani na kazini. Kazi hufanya sehemu kubwa ya maisha yetu.”

Dk. Godwin alisema sheria ya afya ya akili, bado haijaegemea katika masuala ya afya ya akili mahali pa kazi, ili kuweka masuala hayo kisheria, kama vile kutoa huduma ya kwanza ya afya ya akili iwapo kuna hitaji hilo kazini.

Alisema kuelekea Siku ya Afya ya Akili Duniani, kila jamii, mwajiri na mwajiriwa ni muhimu kuangalia wajibu wao, ili kulinda afya ya akili, kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi.

“Historia inaonesha ni suala muhimu katika elimu hii, inabidi tulizungumzie kwa sababu utafiti namba zinaonesha kuna tatizo kuhusu suala la afya ya akili mahali pa kazi.

Utakuta kuna watu wanafanya kazi mtandaoni, wapo wameajiriwa huko, je, bosi anakutreat vipi. Au kama umejiajiri mazingira yako yakoje? Labda unapokea matusi mtandaoni vyote hivyo vinahitaji kuzungumza kama kazi ya mtandaoni inakuletea kipato kuna tatizo, kuna haja ya kulizungumzia.”

Mwanasaikolojia kutoka Hatua Therapies, Jestus August, alisema katika mahala pa kazi kumtambua mfanyakazi bora mbele ya hadhira ni jambo jema, ingawa kwa baadhi ya wafanyakazi huwa chanzo cha magonjwa ya akili kama vile sonona.

Alisema pia mahala pa kazi iwapo miongoni mwa wafanyakazi mwenzako amekukosea si vyema kumsema kwa watu, badala yake mhusika afuatwe kwa lugha ya kirafiki.

“Ni muhimu kuwa na ‘mentors’ washauri, kuna wakati mabosi wetu wanatukosea, wafanyakazi wenzetu wanatukosea, malipo hayaturidhishi hivyo ili kupona na kuwa na afya ya akili yenye utengamao kuna haja ya kuwa na ‘mentors’ hawa ni zaidi ya walimu ili kutuweka sawa,” alisema mwanasaikolojia huyo.

Alisema mahali pa kazi pia vijana huathiriwa zaidi, kama vile kuegemea katika ushabiki wa timu za michezo ya aina tofauti, huku wakitoa kauli zisizofaa kulingana na mazingira walioko, wakijisahau kwamba eneo hilo ni mahali pa kazi.

“Kuna ambao wanavaa tofauti mahali pa kazi, anaambiwa usivae viatu vua michezo yeye anavaa mahali pa kazi. Kingine ni kutamani kuweka malengo binafsi hasa kwa waliotoka vyuoni kutaka maendeleo ya haraka kuliko aliowakuta kazini.

Kijana anakuwa na matarajio makubwa kwamba anawaza awe na mshahara mkubwa, awe na safari nyingi za nje, apendwe sana na bosi, asafiri nje sana, hayo matarajio hayo yanamfanya atamani makubwa, asipopata mambo yanaharibika, anadhani kazi hii ndio italeta mafanikio kwa ukoo, familia yote, huku mshahara kidogo, unavuruga afya ya akili,” alisema August.