Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2024, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mkoa wa Kihuduma DAWASA Mbagala wameanza maadhimisho hayo kwa kuwatembelea wateja wake wa maeneo ya Vijibweni katika mtaa wa Mianzini na kata ya Kilungule mtaa wa Kwa Mzungu kwa lengo la kuboresha na kuimarisha huduma zake.
Akizungumzia zoezi hilo Meneja Mkoa wa Kihuduma DAWASA Mbagala,Judith Singinika amesema zoezi hilo limelenga kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Mamlaka na wateja wake sambamba na kutatua changamoto mbalimbali za kihuduma wananchi zitakazo saidia boresha huduma.
"Leo maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja na tumejipanga kupita mtaa kwa mtaa na kuzungumza na wateja wetu ili tuweze kupata mrejesho wa huduma zetu sambamba na kuimarisha mahusiano tuliyonayo na wateja wetu, kitu ambacho kitatusaidia kuboresha huduma zetu" amesema Singinika
Nae Salma Rashid mkazi wa mtaa wa Mianzini kata ya Vijibweni ameipongeza na kuishukuru DAWASA kwa kuwafikia katika mitaa yao na kuwasikiliza kitendo ambacho kitasaidia kuboresha mahusiano pamoja na utendaji kazi wa watumishi wa mamlaka katika kutatua changamoto za wateja.
Wiki ya huduma kwa wateja imeadhimishwa rasmi tarehe 7 Oktoba, 2024 na kuhitimishwa tarehe 11 Oktoba, 2024 kila mwaka iliyobeba kauli mbiu ya zaidi ya Matarajio.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED