Laini za simu milioni 35 zaunganishwa intaneti

By Allan Isack , Nipashe
Published at 07:24 AM Sep 21 2024
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa
Picha:Mtandao
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema laini za simu za mkononi zaidi ya milioni 75 zinatumiwa na Watanzania kwa ajili ya mawasiliano, huku laini milioni 35 zikiunganishwa moja kwa moja na huduma ya mtandao wa intaneti.

Waziri Silaa alibainisha hayo jana jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Connect 2 Connect lililowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa kupitia kongamano hilo, watajadiliana kuunganishwa kidigiti kusiwe tu  kupata Intaneti, bali kuwapo uhakika wa huduma yenye kasi, isiyokuwa na hitilafu na kwa gharama nafuu kwa watumiaji.

"Tumewakutanisha wadau kujadiliana kuhusu mafanikio tuliyoyapata kwa kuwaunganisha wananchi na itaneti, pia kuangalia njia za kufikia muunganiko bora zaidi ya huu tuliokuwanao sasa ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii," alisema Waziri Silaa.  

Waziri huyo alisema kuwa kutokana na kazi iliyofanywa na serikali, wamefanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa mfumo wa 3G kwa asilimia 89, 4G kwa asilimia 83 na 5G kwa asilimia 15.

Alisema kwa hali ya dunia hivi sasa intaneti imebeba maisha ya watu kwa kuwa shughuli nyingi, zikiwamo za kilimo na biashara zinafanyika huko.

Alisema kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na mawasiliano, serikali imejipanga kuhakikisha minara ya mawasiliano inasimikwa ili kurahisisha upatikanaji huduma hiyo kwa wananchi.

"Serikali Mei 2023 ilizindua mkakati wa ujenzi wa minara 758 kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili tupeleke huduma kwenye maeneo ambayo hayana," alisema.

Waziri Silaa alisema mbali na minara 758, kuna minara mingine 636 inajengwa na mradi utaanza Oktoba mwaka huu kuhakikisha maeneo yote nchi yanapata mtandao wa simu, intaneti, redio na televisheni.

Kuhusu hali ya usalama wa kimtandano, waziri huyo alisema Tanzania iko vizuri kwa kuwa ni moja ya nchi zilizowekeza vizuri kwa kuwa kuna kitengo cha kudhibiti uharamia wa mawasiliano ndani ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kinachosimamia masuala ya kimtandao na kuratibu masuala ya usalama wa kimtandao katika kila sekta.

"Serikali itahakikisha Watanzania wanafanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kupitia kwenye mitandao wanakuwa salama kwa kuwa tuna mifumo imara ya kimtandao," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Helios Towers, Gwakisa Stadi, alisema kampuni hiyo nchini inasimamia minara zaidi ya 400 na wana wateja zaidi ya 10,000 ambao ni watumiaji wa minara hiyo.

Alisema kazi kubwa ya mirana hiyo ni kuunganisha huduma za mawasiliano na wateja wao wakubwa ni kampuni za mawasiliano ya simu, kampuni za usambazaji intaneti na televisheni zilizoweka vifaa vyao vya mawasiliano kwenye minara hiyo.

"Kazi yetu kubwa tunaunganisha, kujenga na kusimamia minara na tumedhamini kongamano hili, kwa kuwa maono ya kampuni yetu ni kuwaunganisha Watanzania na mataifa mengine ya Bara la Afrika na nchi za Mashariki ya Kati," alisema mkurugenzi huyo.