Wanavuja machozi kisa vijana hawaoi, hakuna watoto wanaozaliwa

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 05:33 PM Apr 07 2024
Wanavuja machozi kisa vijana hawaoi.
PICHA: MAKTABA
Wanavuja machozi kisa vijana hawaoi.

IKO kasumba ya vijana hivi sasa kutotaka kuoa na wengine kuolewa, wakiishia kuamini kuwa ‘single mother’ ni bora zaidi ya kuishi na mume.

Kauli zao siku zote ni kwamba “siwezi kuoa kama sina vitu vya thamani ndani. Hata  wanawake wa sasa, ni ngumu kukubali kuolewa na mwanamume asiye na kitu.

“Kwa umri wangu, si kama sitaki kuoa, lakini siwezi kuingia kwenye ndoa kama sina gari, nyumba, biashara, kitanda, jokofu, kabati na vitu vingine vya thamani.”

Basi katika kutafuta mali pamoja na mwanamke atakayemuoa, vijana walio wengi wanaeleza bila kumung’unya maneno kwamba hakuna mwanamke anayeweza kumvumilia mwanamume asiye na kitu ndiyo maana nao hawataki kuoa.

Wanaoijua Biblia, kupitia kitabu cha Ayubu 15:20 imeandika: “Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote, hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye kuonea.” Kwa maana hiyo, uchungu husababisha mambo ya mtu kuwa magumu na uchungu husababisha kufikiri machungu zaidi kuliko mema.

Jambo lingine ni ulevi uliopindukia. Watu wanasahau kwamba uamuzi wao wa kutotaka kufanya kazi za uzalishaji mali na kujikita katika ulevi kucha kutwa, nalo ni kiini cha kupoteza nguvu na uwezo wa kuwa na mwanamke.

Nimeanza kuleza hayo kwa sababu ya jambo linaloumiza kichwa. Huko  Mwika Kaskazini, Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, inadaiwa ndoa ni hadithi nyingine.

Serikali ya eneo hilo imekiri hadharani kwamba hakuna vijana wanaooa, wala watoto wanaozaliwa Mwika Kaskazini kwa sasa kutokana na mambo mbalimbali yanayochangia tatizo hilo. Ni hali ya kustaajabisha inayoelezwa na Ofisa Mtendaji Kijiji (VEO) cha Msae-Kinyamvuo katika Kata ya Mwika Kaskazini, Elizabeth Mkony.

Kutokana na tishio hilo, Halmashauri ya Kijiji kwa kushirikiana na viongozi wa dini, wamekubaliana kuja na mpango kabambe wa kupambana na changamoto ya kuporomoka kwa maadili, kunakosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya na pombe kupita kiasi.

“Sasa hivi, Mwika Kaskazini hakuna vijana wanaooa wala watoto wanaozaliwa. Kanisani nako kwa mwaka mzima unakuta si zaidi ya watoto watatu wanatangazwa kuzaliwa na kubatizwa.

 “Tumefikia hatua ambayo jamii inaumia, wengine wana kufa vifo vya ajabu kwa sababu ya ulevi. Vijana wanashindwa kufanya kazi za kujitolea kwa sababu ya kukosa nguvu.

“Kutokana na hali hii kushamiri, kama uongozi wa kijiji pamoja na viongozi wa dini kufanya jambo, ili kuwanusuru vijana wetu na kuongeza uzazi. Kwa vile tunaona kwa miaka miwili ijayo, kuna uwezako wa kukosa vijana.”

Badhi ya mambo yanayowekewa mkazo na timu hiyo ya pamoja, ni kutoa elimu na kukemea ulevi kupindukia, ubakaji, ulawiti, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi ya dawa za kulevya na wanafunzi kukatisha masomo.

Kabla ya kutangazwa kwa azimio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Wilbad Mariki, anasema: “Hakuna namna, imebidi tukae na viongozi wa dini na kuweka mikakati ya jinsi ya kupambana na hali mbaya iliyopo.

“Kata nzima ina watu 19,000 hata 30,000 hatujaikaribia. Tunazidi kuporomoka, tunaona tusipopambana wote kwa pamoja kuona mambo yanaenda vizuri, hatutakuwa na kizazi kinachofanya kazi,“ anasema. 

Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Mwongai wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Neema Malisa, anasema wakiwa viongozi wa dini wameanza kuchukua hatua kwa nafasi yao.

“Tunawafundisha watu wetu faida za kumpenda Mungu, na hasara za kujiingiza katika matendo maovu kama ushoga, ulawiti, ulevi, ubakaji na matumizi ya dawa za kulevya.

“Ni vile tu mtu hawezi kuona, lakini tunaumizwa sana na mambo mabaya yanayotendeka katika jamii. Tuko tayari kuungana na serikali kuhakikisha mambo maovu na haramu hayaingii kwenye kijiji chetu.

“Mnafurahi watoto wetu wanapokufa, mnafurahi watoto wetu wanapoacha kuoa na kujikuta wanaingia kwenye ushoga na ulawiti? mimi naona tuiunge mkono serikali. Sisi viongozi wa dini tuko tayari,” anasema Mchungaji Malisa.

Kwa kweli hali hii nim baya na iwapo itaachwa jinsi ilivyo, kuna hatari ya jamii kukosa kizazi. Si kizazi tu bali kizazi madhubuti ambacho kitaendeleza kupeleka mbele gurudumu la maendeeo. Mungu atusaidie.   

·         Godfrey Mushi, ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa simu namba 0715 545 490 au barua pepe: [email protected]