Majaliwa ataka elimu utambuzi wasio raia

By Adela Madyane , Nipashe Jumapili
Published at 08:33 AM Jul 21 2024

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amelitaka Jeshi la Uhamiaji kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwatambua na kutoa taarifa za watu ambao si raia wa Tanzania katika kila kituo cha uandikishaji.

Aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura uliofanyika katika viwanja vya Kawawa vilivyoko Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Alisema mwananchi ndiye mtu wa kwanza kutambua nani ni mtanzania na nani si mtanzania katika maeneo wanamoishi.

Majaliwa aliagiza kuwapo ushirikiano baina yao ili kutambua wasio na sifa ya utanzania hawajiandikishi katika daftari hilo na kufanya mchakato huo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Watanzania lazima tuwe wazalendo, upigaji kura ni kwa sisi watanzania, tunachagua viongozi watakaoliongoza taifa. Tunachagua viongozi ambao watakuja kuwa viongozi wa mitaa yetu na vitongoji vyetu, kwanini kuruhusu mtu wa nje aje atupigie kura?

“Atatuamlia ambavyo sisi hatutaki, kwahiyo tusiruhusu mtu yeyote kutoka nje ajiandikishe katika daftari la mpigakura” aliagiza.

Majaliwa alisema kila mtanzania asimamie mchakato huo kwa uadilifu, kwa kutoa taarifa sahihi za raia anayetaka kujiandikisha ambaye si mtanzania.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuweka mawakala watakaosimamia mchakato huo kutoka katika kijiji husika kwakuwa ndio wanaowafahamu wananchi wa maeneo yao, na hivyo kuwa rahisi kutambua ambao hawana sifa za kuandikishwa kama raia wa Tanzania.

“Ninaomba mawakala wote muwe wazalendo na makini kuangalia kila anayekuja kuboresha taarifa zake na kufuatilia namna anavyohojiwa, kwakuwa maelezo yake yanaweza kutusaidia kutambua aliye raia na asiye raia,” alisema.

Majaliwa aliwataka watendaji na wote watakaohusika katika mchakato huo kutumia lugha lugha na kutekeleza wajibu huo kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotolewa na tume na kuhakikisha unakamilika bila kuwa na dosari yoyote.

Kwa upande wa asasi zilizopata vibali vya kutoa elimu, Waziri mkuu Majaliwa alisema zinapaswa kutoa elimu sawasawa na makubaliano yaliyowekwa katika mwongozo na kwamba, wasivunje sheria nyingine za nchi kwa kigezo cha kuwa na kibali cha kutoa elimu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndariananga, alisema mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akitoa taarifa ya Tume Huru ya Uchaguzi, Mwenyekiti wake, Jacobs Mwambegele, alisema mchakato wa kuboresha au kuhamisha taarifa kwa njia ya kieletroniki umeboreshwa katika simu zote.

Jaji Mwambegele alisema asasi 157 zimepewa vibali vya kutoa elimu hiyo huku  asasi nyingine 33 za ndani na nane za kimataifa zikipewa vibali vya kuwa waangalizi wa uandikishaji kwa ajili ya kutazama uendeshaji wa mchakato huo.

Alisema taasisi hizo zilizopewa vibali zimepewa nyaraka mbalimbali ikiwamo Katiba, sheria na miongozo inayosimamia jukumu la utoaji elimu ya mpigakura na utazamaji.