UMAHIRI ulionyeshwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya St Anne Marie Academy kwenye kuzungumza lugha mbalimbali kumewashangaza wazazi walihudhuria mahafali ya shule hiyo mwishoni mwa wiki.
Wanafunzi hao walionyesha vipaji vyao jana Jumamosi kwenye mahafali ya 20 ya shule ya sekondari shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi hao walionyesha umahiri kwenye kuelezea masuala mbalimbali ya kitaaluma kwa kutumia lugha ya kingereza fasaha, kikifaransa hali ambayo iliwafanya wazazi waliohudhuria mahafali hayo kulipuka kwa shangwe .
Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ya 20 ni Mbunge wa Bukene CCM, Jummane Selemani Zedi aliyeambatana na Mkurugenzi wa mtandao wa shule za St Anne Marie Academy, Dk. Jasson Rweikiza.
Mmoja wa wazazi aliyehudhuria mahafali hayo yanayoendelea, Halima Kitonka alisema uwezo wa wanafunzi hao unaonyesha namna walivyoandaliwa vyema na walimu mahiri.
"Kuzungumza Kifaransa na kingereza kwa ujasiri namna ile ni jambo ambalo limenifurahisha sana kwa kweli na tunajua umuhimu wa lugha za kigeni duniani kwa hiyo badala ya kukazania kingereza tu ni vyema tukaiga hawa St Anne Marie kuwafundisha wanafunzi lugha zingine kama kifaransa na kichina," alisema Halima
Alisema pia amefurahishwa kuona namna wanafunzi wa shule hiyo walivyoonyesha umahiri wa kuelezea masuala ya kitaalamu kama vile ni wahandisi tayari.
Mzazi mwingine, Nathaniel Rwezaura, alisema amefurahi sana kuona wanafunzi wa shule hiyo wanajiamini katika kuzungumza lugha zote kwa ufasaha na bila kubabaika.
“Wamemudu sana kuelezea masuala mbalimbali ya kitaaluma na unaweza ukadhani kwamba ni watu ambao wako kazini kutokana na umahiri wao nawapongeza sana walimu wa St Marie kwa kufanyakazi usiku na mchana kupata mafanikio haya,” alisema
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED