Benki ya Dunia yaridhishwa hatua uandaaji dira 2050

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 05:34 PM Jan 12 2025
MKURUGENZI wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Nathan Belete.
Picha: Mpigapicha Wetu
MKURUGENZI wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Nathan Belete.

MKURUGENZI wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Nathan Belete, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuandaa rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Akizungumza jana katika mkutano wa ushirikiano na washirika wa maendeleo wa kuhakiki rasimu hiyo, uliofanyika mkoani Dar es Salaam, Belete alielezea kuridhishwa kwake na kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Mipango na Uwekezaji.

Katika hotuba yake, Belete aliainisha vipengele muhimu ambavyo vinaweza kuboreshwa zaidi ili kuimarisha dira hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuweka msisitizo katika hifadhi ya jamii. 

"Uwezo wa nchi kukua kwa njia shirikishi unahusiana moja kwa moja na jinsi hifadhi ya jamii inavyozingatiwa," alisema.

Hata hivyo, aliangazia changamoto ya kuhakikisha kwamba mifumo ya hifadhi ya kijamii inapata ufadhili endelevu, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa sera hizo.

Belete pia aligusia mabadiliko ya tabianchi, akipongeza juhudi za serikali za kuingiza suala hilo kwenye dira ya maendeleo.

"Mabadiliko ya tabianchi hayapaswi kushughulikiwa tu katika sekta chache za uzalishaji, bali inapaswa kuzingatiwa katika kila sekta," alisema.

Pia alieleza kuwa mikakati bora ya kushughulikia changamoto za tabianchi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Vilevile, alitoa changamoto kwa serikali kuzingatia nafasi ya Tanzania katika ushirikiano wa kikanda, akisema hilo ni eneo lenye fursa kubwa. "Suala la ushirikiano wa kikanda, hasa kwenye vipengele vya biashara, linapaswa kupewa kipaumbele zaidi na kuendana na mpango wa uwekezaji wa umma”.