COREFA yawaaga vijana 16 wanaojiunga na kambi ya FIFA, TFF

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 06:05 PM Jan 12 2025
COREFA yawaaga vijana 16 wanaojiunga na kambi ya FIFA, TFF.
Picha: Mpigapicha Wetu
COREFA yawaaga vijana 16 wanaojiunga na kambi ya FIFA, TFF.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kimefanya kikao maalum na wazazi pamoja na watoto 16 walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuwaaga na kuwaombea heri wanapoelekea kujiunga na kambi ya mafunzo inayoendelea mkoani Tanga kwa muda wa wiki moja.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za COREFA zilizopo Kibaha kwa Mathias, ambapo mbali na kuwaaga watoto hao, viongozi wa COREFA walihakikisha wazazi kuhusu usalama wa watoto wao na kueleza umuhimu wa kambi hiyo katika kukuza vipaji vyao.

Mwenyekiti wa COREFA, Robert Munisi, amesema mpango huu wa kuendeleza vipaji kwa vijana umeanzishwa na FIFA kwa kushirikiana na TFF, huku COREFA ikiwa mtekelezaji wa mpango huo kwa Mkoa wa Pwani.

1

"Kupatikana kwa vijana hawa 16 ni matokeo ya mchakato wa kuchagua vipaji uliofanywa na FIFA na TFF kwa kushirikiana na vituo vya michezo vilivyopo Pwani. Vijana hawa walichaguliwa kati ya wenye umri wa miaka 11 hadi 14, na baadaye waligawanywa kwenye Kanda ya Kusini na Kanda ya Kaskazini," alisema Munisi.

Mmoja wa vijana walioteuliwa, Rashid Shamte, amewashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono na kuonyesha kipaji chake, huku akiahidi kufanya vizuri katika kambi hiyo ili kutimiza ndoto zake.

Aziz Mwashambwa, mzazi wa Edmund, ametoa shukrani kwa FIFA na TFF kwa juhudi zao za kugundua vipaji vya watoto na amewataka wazazi kufungua milango kwa watoto wao kushiriki michezo ili kuonyesha vipaji vyao.

Mpango huu unalenga si tu kukuza vipaji vya michezo nchini bali pia kuwajengea vijana uwezo wa kushindana kimataifa katika siku zijazo.