NI wiki ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hii ni kwa sababu ni wiki ya kupata viongozi waandamizi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Aidha, uchaguzi wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake ngazi ya taifa ni Jumanne ijayo wakati hatima ya Katibu Mkuu, John Mnyika na Manaibu wake, itajulikana Januari 22, mwaka huu.
Juzi na jana, Kamati Kuu ya chama hicho imekutana Dar es Salaam, kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye mabaraza ya chama hicho ya Vijana (BAVICHA), Wanawake (BAWACHA) na Wazee (BAZECHA), kati ya 303 waliojitokeza.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, alisema kwa siku ya jana, kamati hiyo imefanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za BAWACHA Taifa.
Alisema wagombea 93 wamejitosa kuwania nafasi ndani ya baraza hilo la wanawake, BAVICHA (69) na BAZECHA (85).
Alisema idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza ndio imesababisha Kamati Kuu, kutumia siku mbili kuwahoji na kuteua.
“Kamati Kuu inaendelea na vikao vya uchujaji na uteuzi wa wagombea ambayo ilianza jana (juzi), leo (jana), tunafanya usaili wa BAWACHA Taifa,” alisema.
Mrema alisema mchakato wa uchaguzi ndani ya mabaraza hayo unaendelea vizuri na kwamba leo Kamati ya Utendaji ya BAVICHA itakutana kwenye kikao cha kuandaa Mkutano Mkuu utakaofanyika kesho Jumatatu katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
“Uchaguzi wa Baraza la Wazee nao utafanyika keshokutwa. Uchaguzi wa Baraza la Wanawake utafanyika tarehe 16 (Alhamisi). Baada ya hapo tutakuwa na vikao vingine vya kuhoji na kuchuja wagombea wa nafasi za chama Taifa (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti),” alisema.
Alisema kwenye uchaguzi wa mabaraza watapatikana wajumbe wapya wa Kamati Kuu, akitoa mfano wa BAVICHA ambako Mwenyekiti wake wa sasa, John Pambalu, amemaliza muda wake na hana sifa za kugombea tena.
Kutokana na hilo, Kamati Kuu itakayowateua Mbowe na Lissu, itakuwa na sura mpya.
“Ikumbukwe kwamba watakaochaguliwa kuwa Wenyeviti kwenye mabaraza wanakuwa wajumbe wa Kamati Kuu. Kwa hiyo wako wajumbe wapya watakaoingia. Mfano ni Mwenyekiti mpya wa BAVICHA, atashiriki kuteua wagombea wa nafasi ya chama Taifa,” alisema.
Alisema baada ya uteuzi wa wagombea wa Mwenyekiti na Makamu wake, majina yatapelekwa Baraza Kuu na kisha Mkutano Mkuu Januari 21, 2025.
Mrema alisema baada ya uchaguzi mkuu, Baraza Kuu la CHADEMA litakutana tena Januari 22, kwa ajili ya kuteua Katibu Mkuu, Manaibu wake na wajumbe nane wa Kamati Kuu.
Kwa siku hizo mbili, kikao cha Kamati Kuu kinaongozwa na Mbowe anayegombea kutetea nafasi yake kwa mhula mwingine, akisaidiana na Lissu ambaye amejitosa kutaka kumng’oa kwenye kiti hicho. Mgombea mwingine aliyejitosa kwenye Uenyekiti ni Charles Odero.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wanaowania kurithi nafasi ya Lissu, Ezekia Wenje na John Heche, ambaye alitangaza kuwa upande wa Lissu.
WAGOMBEA BAZECHA
Januari 07, mwaka huu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari, alisema wagombea katika nafasi ya uenyekiti wa Bazecha Taifa, ni Hashim Juma Issa, John Mwambigija, Hugo Kimaryo, Mwecha Tiba na Suzan Lyimo.
Katika nafasi ya Katibu Mkuu, wagombea wako watatu ambao ni Dk. Leonard Mao, Hellen Mayanza na Kasmiri Mabina, wakati katika nafasi ya naibu katibu mkuu (Bara), waliojitokeza ni Hamid Mfaligundi na Omary Mkama na kwa upande wa naibu katibu mkuu (Zanzibar) ni Rajab Hamis Bakari na nafasi ya mweka hazina ni Florence Kasilima.
BAVICHA
Kwa upande wa Bavicha, waliojitokeza kugombea uenyekiti ni Deogratius Mahinyila, Hamis Masoud na Shija Shibesi.
Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti (Bara), wagombea ni Vitus Nkuna, Baraka Charles, Necto Kitiga, Juma Ng'itu, Nice Sumari na Mkola Masoud.
Nafasi ya makamu mwenyekiti (Zanzibar), wagombea ni Abdallah Haji na Kassim Abdallah. Katibu mkuu ni Benjamin Nteje, Idrisa Kassim, Ambokile Mwangosi, Dua Lwamzito na Sheila Mchamba.
Waliojitokeza nafasi ya naibu katibu mkuu (Bara) ni Emmanuel Kasturi, Mussa Bashar na Levin Mbughi, wakati nafasi ya naibu katibu mkuu (Zanzibar) ni Awena Nassoro na Said Abdulla Khamis. Nafasi ya mratibu wa uhamasishaji wamejitokeza wagombea wawili, Felius Kinimi na Dedan Wangwe.
Kwa upande wa Mweka hazina wagombea ni Michael Materu, Badi Ibrahim, na Ramna Abdallah.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED