USIKU wa deni haukawii, wawakilishi wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa, Simba na Yanga zitashuka katika viwanja viwili tofauti ugenini leo ili kucheza mechi zitakazoamua hatima ya nafasi yao ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wao watawavaa Al Hilal katika mechi ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kuanzia saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa De la Capitale nchini, Mauritania huku Bravos do Maquis ya Angola ikiwakaribisha Simba kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho kuanzia saa 1:00 usiku.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema amekiandaa vyema kikosi chake kwa ajili ya kupambana bila kumwangalia mpinzani anacheza vipi.
Kocha wa Yanga, Ramovic, amesema tayari amekiandaa kikosi chake kwa ajili ya mchezo huo, akitarajia kupata matokeo mazuri licha ya ubora wa wapinzani wao.
"Kikosi kiko tayari, nimekiandaa kwa ajili ya kucheza mechi, simwangalii mpinzani ili kuwa bora, napambana kuhakikisha nashinda mchezo, ninachokifurahia zaidi ni namna timu yangu inavyoimarika na ipo kwenye morali nzuri, hivyo naamini kila kitu kinawezekana kwa kushindana," alisema kocha huyo.
Meneja wa Yanga, Walter Harrison, alisema katika mchezo wa leo kikosi chao kimepata na mashabiki wengi, ambao wameahidi kwenda kuwashangilia uwanjani kwa sababu baadhi ya wachezaji wanatoka nchi za Afrika Magharibi.
"Tumepata sapoti ya baadhi ya mashabiki kwa sababu baadhi ya nyota wetu wanatokea kwenye ukanda huu wa Afrika Magharibi, Djigui Diarra huku ni maarufu sana na amekuwa na wapenzi wengi hapa, hasa ikizingatiwa hizi nchi ni majirani, yaani amekuwa ndiyo kama mwenyeji wetu. Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua nao wamekuwa kivutio kikubwa sana, imetufanya tuwe na mashabiki wengi na leo watakuwa uwanjani kutushangilia, tutakuwa kama tupo nyumbani tu," alisema Harrison.
Ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo, Yanga inapaswa kushinda mchezo huo na hii imekolezwa na mpinzani wake mkubwa, MC Alger ya Algeria kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).
Matokeo hayo yamewafanya MC Alger kufikisha pointi nane, hivyo Yanga itakuwa ikisaka ushindi kwa udi na uvumba ili kufikisha pointi saba, lakini pia ikihitajika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Waarabu hao hapa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Naye Kocha Mkuu wa Al Hilal, Florent Ibenge, ambaye timu yake imeshafuzu hatua inayofuata, alisema anaweza kubadili kikosi chake katika mechi ya leo na kupanga baadhi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi kwenye michezo iliyopita kwa ajili ya kulinda nguvu kuelekea hatua ya robo fainali.
"Kwa sasa tunayo nafasi ya kupumzika kidogo na kujiandaa kwa hatua inayofuata. Hatuwezi kupuuza umakini, lakini ni muhimu pia kuhakikisha wachezaji wangu wanakuwa na nguvu za kutosha kwa changamoto kubwa zilizo mbele yetu.
Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa na umuhimu mkubwa kwao, lakini kwa upande wetu, tunahitaji kujiandaa kwa hali yoyote. Siwezi kujivunia mapema. Wachezaji wangu watahitaji kupumzika kidogo kabla ya michezo inayofuata," alisema kocha huyo.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi wataingia uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi na si sare kwa sababu timu kubwa kama yake haiwezi kujiandaa kugawana pointi na mpinzani.
“Tunahitaji sare kufuzu, na ushindi ili kuongoza kundi. Sisi siyo timu ya kucheza kusaka sare, tutajitahidi kushinda mechi. Lakini tunahitaji walau sare na ushindi mmoja katika mechi zetu mbili zilizobaki au kushinda zote.
Tunapaswa kuwa makini sana, Bravos wanacheza mechi kwa fujo, yaani kushambulia zaidi. Nadhani tunapaswa kucheza tofauti na wanavyopenda wao, tucheze tofauti na tulivyocheza mechi ya CS Sfaxien. Tunapaswa kuitawala mechi zaidi, tukiwa na mpira na bila mpira," alisema Fadlu.
Kocha huyo alisema kitu ambacho kitakuwa faida kwao ni hali ya hewa ya Luanda ambayo haitofautiani na ile iliyoko Dar es Salaam.
"Tunafurahi tumepata mapokezi mazuri kutoka kwa watu wa Angola, timu ipo katika hali nzuri. Hali ya hewa ni kama Dar es Salaam, tupo tayari kwa mchezo," Fadlu alisema.
Kiungo wa Wekundu wa Msimbazi, Debora Fernandes, ambaye ni raia wa nchi hiyo, amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu anafahamu ubora wa Bravos do Maquis inapokuwa nyumbani, lakini hiyo haiwezi kuwafanya wasitimize malengo yao.
"Utakuwa mchezo mgumu, natambua wanacheza nyumbani na wanahitaji pointi tatu, ila malengo ya Simba yanajulikana, ni kuhakikisha tunafanya vizuri," kiungo huyo alisema.
Mario Soares, Kocha Mkuu wa Bravos do Maquis, ameliambia gazeti hili mechi hiyo itakuwa nzuri na ngumu, huku akisema wanakwenda kucheza na timu yenye wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kuimaliza mechi, huku akimhofia zaidi, Jean Ahoua.
"Ina wachezaji wazuri, ni ngumu kumtaja kila mmoja kwa jina, ila mmoja wao ni yule mwenye jezi namba 10, kwangu huyo ndiyo hatari zaidi, anacheza taratibu tu, lakini mipira yake ni hatari sana," alisema kocha huyo.
Simba inahitaji sare tu katika mchezo wa leo ili kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi A, kwa sababu itafikisha pointi 10 ambazo hata kama Bravo do Maquis watafikisha kwa kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia na Wekundu wa Msimbazi wakapoteza dhidi ya CS Constantine, bado watakuwa wamefuzu kutokana na matokeo ya walivyokutana wenyewe kwa wenyewe. Ikumbukwe katika mchezo wa kwanza ulichezwa Novemba 7, mwaka jana hapa nyumbani Mnyama alipata ushindi wa bao 1-0.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED