Ajali daladala ilivyoua mmoja, kujeruhi wanne

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 09:48 AM Jan 12 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilibroad Mutafungwa.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilibroad Mutafungwa.

MWANAMKE mmoja ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja, anayedhaniwa kuwa na umri kati ya miaka 20 hadi 25, amefariki dunia katika ajali iliyohusisha daladala kugonga magari matatu.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilibroad Mutafungwa, alisema ilitokea juzi majira ya saa 1:00  asubuhi katika eneo la Iseni, Kata ya Butimba, wilaya ya Nyamagana. 

Alisema ajali ilitokea katika barabara ya Kenyatta ambako gari lenye namba za usajili T. 207 DQZ aina ya Toyota Coster likitokea Nyegezi kwenda Mwanza mjini, liligonga gari yenye namba za usajili T. 876 DDA Toyota IST. 

Kamanda Mutafungwa alisema gari hilo aina ya IST lililokuwa likiendeshwa na Costantinius Mabele (32), Mfanyabiashara na Mkazi wa Mkolani, liligonga gari lingine lenye namba za usajili T. 571 DND aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea Mwanza mjini kwenda Nyegezi.  

"Katika ajali hiyo mtu mmoja jinsia ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 25 amefariki dunia na watu wanne wamejeruhiwa," alisema DCP Mutafungwa.

 Kamanda Mutafungwa aliwataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Maua Rashid (30), Mkazi wa Buhongwa, Fabiani Ndalo (50), Hadija Mussa (24), mkazi wa Kiloleli na David Mussa (27), Mkazi wa Kiseke ‘A’.

 Alisema wamepelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Bugando na kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari yenye namba za usajili T. 207 DQZ kuyapita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa bila kuchukua tahadhari.

 Pia alisema baada ya ajali hiyo dereva wa gari hilo alitokomea kusikojulikana na kuwa Jeshi hilo limeanza msako wa kumtafuta dereva huyo ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

 "Tunawakumbusha watumiaji wa barabara kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani kwani hatutasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuvunja sheria hizo," alisema DCP Mutafungwa.