Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Chona, Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, wamechangisha zaidi ya Shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Chona.
Lengo la ujenzi huu ni kuwanusuru wanafunzi wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni zinazokatisha masomo yao.
Shule hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2007, inahudumia wanafunzi kutoka vijiji vya Chona, Busenda, Itebele, Ishila, Nhimbo, Nsalaba, na Nshimba. Vijiji hivi vipo umbali wa takriban kilomita 10 kutoka shule hiyo, hali inayowalazimu baadhi ya wanafunzi kupanga mitaani ambako hukumbana na changamoto za kurubuniwa na vijana, kujiingiza katika mahusiano, na hatimaye kupata ujauzito.
Akizungumza wakati wa harambee iliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo, Mbunge Cherehani alionya kuwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi ni kosa la kisheria linalostahili adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela. Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili wanafunzi waweze kufikia ndoto zao bila vikwazo. Alieleza kuwa ujenzi wa bweni hilo ni sehemu ya juhudi za pamoja na wananchi kuhakikisha usalama wa wasichana na kuwapa mazingira bora ya kusoma.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chona, Masamaki Madaha, alieleza kuwa wanafunzi wengi hukatisha masomo kutokana na changamoto za ujauzito. Hali hii inatokana na umbali wa vijiji wanakotoka na mazingira magumu ya kupanga mitaani. Alisema kuwa jitihada za kushirikiana na sungusungu zimeanzishwa ili kudhibiti tatizo hili na kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza masomo yao salama.
Madaha alibainisha kuwa mwaka jana, kati ya wanafunzi 241 wa kidato cha kwanza walioandikishwa, ni 170 pekee waliobaki shuleni, huku 71, wengi wao wakiwa wa kike, wakiacha masomo.
Mwanafunzi wa kidato cha pili, Limi Mlekwa, alisema baadhi yao wanalazimishwa kuingia katika mahusiano na vijana wa mitaani, na wale wanaokataa hukumbana na vitisho. Wale wanaokubali mara nyingi hupata ujauzito na kuacha masomo. Aliomba serikali kuhakikisha bweni linakamilika haraka ili kuwapa mazingira salama ya kuishi na kusoma.
Mlekwa pia aliongeza kuwa wazazi wengi wanashindwa kutimiza mahitaji ya watoto wao wanapokuwa wamepanga mitaani, hali inayowasukuma kuingia katika mahusiano kwa sababu ya ukosefu wa chakula na mahitaji mengine. Aliwasihi wazazi kutenga muda wa kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili watoto wao.
Diwani wa Kata ya Chona, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, alisema kuwa vijiji saba vya kata hiyo vimeshirikiana kuchangia ujenzi wa bweni hilo. Kila kijiji kilitoa tripu tano za mawe, huku kila kitongoji kikitoa mifuko mitatu ya saruji. Ushirikiano huu unalenga kupambana na ndoa na mimba za utotoni, ili kuhakikisha wasichana wanapata nafasi ya kumaliza masomo yao bila vikwazo.
Ujenzi wa bweni hilo unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wasichana wa Sekondari ya Chona na kuimarisha azma ya jamii ya kuwapa watoto elimu bora kwa mazingira salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED